Wasimamizi wa vituo na makarani waongozaji kutoka Jimbo la Geita na Busanda wamepewa mafunzo maalum kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024. Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Bomani Geita kwa Jimbo la Geita na katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Butundwe kwa Jimbo la Busanda. Lengo kuu ni kuwawezesha wasimamizi hao kusimamia uchaguzi kwa kuzingatia kanuni, taratibu, na miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Msimamizi Msaidizi, Ndg. Juma Chota, amewasihi wasimamizi na makarani hao kuhakikisha wanazingatia muongozo wa uchaguzi na kufuata taratibu zote wanapotekeleza majukumu yao. Ameeleza kuwa uelewa wa kina wa kanuni za uchaguzi na taratibu za upigaji kura ni muhimu kwa mafanikio ya zoezi hilo.
Aidha, mafunzo hayo yamehusisha maelekezo juu ya utaratibu wa upigaji kura, sifa za wapiga kura, na vifaa vitakavyotumika katika uchaguzi. Washiriki walielekezwa pia namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika vituo vyao vya kazi.
Akifunga mafunzo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Ndg. Karia Rajabu Magaro, amewataka wasimamizi hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuepuka kushurutishwa na mtu yeyote. “Kama hujafahamu jambo fulani, hakikisha unamuuliza kiongozi wako. Ni muhimu kuzingatia kanuni zilizowekwa na kuepuka makosa ambayo yanaweza kuathiri uchaguzi,” alisema Magaro.
Pia, Magaro amewahimiza wasimamizi kuhakikisha maandalizi yote katika vituo yanakamilika mapema ili wananchi waanze kupiga kura kwa wakati, kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni. Alisisitiza kuwa dhamana waliyopewa ni kubwa na wanapaswa kulinda imani hiyo kwa kufanya kazi kwa uadilifu.
Katika hatua nyingine, wasimamizi na makarani hao walikula kiapo cha utii, uadilifu, na uaminifu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Mhe. Devotha Kasebele.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina jumla ya kata 37, vijiji 145, na vitongoji 593. Uchaguzi wa mwaka huu utahusisha vyama saba vya siasa, ambavyo ni CCM, CHADEMA, ACT Wazalendo, CCK, TLP, na ADC.