Na Scolastica Msewa, Kibiti.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava ameeleza kuridhishwa na utekelezwaji wa miradi 15 wilayani Kibiti mkoa wa Pwani baada ya kutembelea, kukagua na kuzindua miradi mbalimbali iliyotekelezwa wilayani humo yenye thamani ya zaidi ya shilingi billion 2.4 za kitanzania.
Akizindua mradi wa shule mpya ya Itonga iliyopo Bungu “A” Mnzava ameupongeza uongozi wa wilaya ya Kibiti kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo kwani ni imani yake kuwa Wanafunzi wanakwenda kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Miradi mingine iliyozinduliwa ni mradi wa barabara ya TARURA, mradi wa majengo ya hospitali ya wilaya, mradi wa maji wa Ruwasa iliyolengwa kumkwamua mwananchi wa Kibiti.
Aidha amekemea tabia ya baadhi ya watu kwenye jamii kuwabagua na kuwanyanyasa watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu.
Mnzava amesema mbali ya unyanyasaji pia wapo wanaoendelea kuwaficha watoto hao na kuwanyima haki zao za Msingi ikiwa ni pamoja na haki ya kupata elimu na kuitaka jamii kuacha tabia ya kuwatenga watoto wenye Ulemavu badala yake wawasimamie wapate haki zao.
Amesema Serikali kwasasa inaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalumu hivyo jamii nayo inatakiwa kuachana na tabia za kuwabagua.
“Nimeisikia hapa Serikali imekuwa ikitoa sh. Milioni 1.3 kila mwezi kwa ajili ya kupata chakula na mahitaji maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, tuendelee kusimamia mahitaji yao muhimu,” amesema.
Aidha amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kundi hilo kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya na huduma nyingine hivyo jamii nayo inatakiwa kuunga mkono juhudi hizo.
Kadhalika ameikumbuaha jamii kuzingatia uendelevu na utunzaji wa mazingira kama ambavyo Ofisi ya makamu wa Rais inavyoelekeza kupanda Milion 1.5 ili kurudisha uoto wa asili.
Amesema shughuli zote za uzalishaji ikiwa ni pamoja na viwanda lazima zizingatie uendelevu na utunzaji wa mazingira.
Awali akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Rufiji Mkuu ya Kibiti Kanal Joseph Kolombo amesema Mwenge huo utakimbizwa km 83.7 ambapo utaifikia miradi ya maendeleo 15 yenye thamani ya shilingi Bililoni 2.4.