Na.Catherine Sungura, Singida
Utekelezaji wa miradi ya barabara katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida upo hali nzuri kwa asilimia 75 ya miradi yote inayotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida Mhandisi Ibrahimu Kibasa amesema Manispaa hiyo ina jumla ya mtandao wa barabara wenye urefu wa Km. 523.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi miwili inayotekelezwa ndani ya Manispaa hiyo, amesema Singida imetengewa bajeti ya barabara yenye jumla ya Shilingi bilioni 2.7.
“Tumetembelea miradi miwili ya barabara ambayo imekuwa ikiendelea kutekelezwa na wakandarasi wetu eneo la hapa mjini,” amesema na kuongeza,
“Miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami eneo la Mnung’una mkataba unagharimu Shilingi Milioni 575,” amesema.
Mhandisi Kibasa amesema ujenzi huo unasimamiwa na mkandarasi JAM contractor unatekelezwa kwa muda wa miezi minane mpaka sasa amefikia 96% ya utekelezaji.
“Ulitakiwa kukamilika 17 Mei, 2024, lakini utamalizika kabla ya muda, amefanya kazi yake kama vile inavyotakiwa.
Amesema mkataba wa pili wa ujenzi wa barabara katika kiwango cha lami eneo la Mwenge-Mungumaji unatekelezwa na Mkandarasi Jp Contractor.
“Umegharimu Shilingi Milioni 611 na ulikuwa ukitekelezwa kwa muda wa miezi sita, umefikia 90% ya utekelezaji, tunatarajia hivi karibuni atamalizia kazi zake na atakabidhi” amebainisha.
Amesema ujenzi wa barabara hizo una tija kwa jamii kwani wamejenga katika maeneo wanakoishi wananchi ambako hapo kabla walikuwa wakipata changamoto lukuki.
“Tuna uhakika tumeboresha maisha ya wananchi, tutakuwa tumeongeza shughuli za ki-biashara na tumepandisha hadhi ya maeneo yao.
“Kwa hiyo hata wale wenye maduka na vitu vyao vilikuwa vikiharibiwa na vumbi kwa sasa thamani ya bidhaa zao zitabaki katika hali halisi.
Ameongeza “Wakala tutaendelea kuboresha barabara za Manispaa na halmashauri nyinginezo kwa kuhakikisha zinakuwa katika ubora.
“Kwa kiwango cha lami, changarawe na kujenga madaraja katika maeneo mbalimbali yaliyo na changamoto.
“Tunashukuru Singida tuna mawe mengi katika mkoa wetu, tunahakikisha tunatumia malighafi zilizopo kwenye eneo husika ili kupunguza gharama za ujenzi,” amesema.
Amesema kwa kutumia rasilimali za ndani ya maeneo husika imekuwa manufaa pia kwa kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
“Kwa hiyo tumekuwa tukijenga madaraja ya mawe katika maeneo mengi katika wilaya nyingi, hata hapa Singida”.
“Singida mjini badala ya kutumia zege peke yake tumekuwa tunatumia mawe, kwa kutumia rasilimali zilizopo na wananchi wanapata Kipato”.
“Wanapeleka watoto shule na maisha mengine yanaendelea, tunaongeza pato la mtu mmoja mmoja.
Mhandisi Kibasa amewasihi wananchi kuendelea kutunza miundombinu kwa ushirikiano wa karibu na viongozi wao katika maeneo yao ili idumu.
“Wawe walinzi wa miundombinu kwa sababu tunaamini zile barabara ambazo zimetengenezwa zimetokana na kodi za wananchi.
“Unapobomoa unaifanya Serikali irudi kutengeneza tena wakati ingeenda eneo jingine au fedha zingeenda kutumika kwenye huduma zingine,” ametoa rai.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa eneo hilo, wamekuwa na mtizamo chanya kuhusu ujenzi huo wa miundombinu.
Wameipongeza TARURA na Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa miundombinu imara.
Mkazi wa eneo la Mwenge Bw. Leonard Kwayu amesema amekuwa hapa tangu mwaka 1998, walikumbana na changamoto nyingi barabarani.
“Walipokuja kuanza kuitengeneza sasa ipo vizuri, mitaro ipo vizuri, changamoto ilikuwa kwa sababu ya udongo. Ilikuwa inachimbika sana ilikuwa na mashimo mengi, sasa hivi serikali inatujali.., tumeona imetujali,” amesema.
Naye Bi. Devotha Charles ameongeza kuletewa lami mtaani kwao, barabara ilikuwa mbaya ilikuwa na mawe sasa imekuwa neema.
“Hata wafanyabiashara tunaonekana vizuri, tunashukuru uongozi wa Mama Samia umetuokoa.
“Itatusaidia kwa biashara zetu hata wagonjwa watasafiri vizuri, barabara imekuwa vizuri,” amesema na kuipongeza TARURA.
“Wamekuwa wepesi kuona hizi barabara za mtaani nasi tumepata lami, waangalie na kwengine ambako hakuna wawawekee lami,” ameomba.