Na Scolastica Msewa, Kibaha.
Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linawashikiria watu wanne kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia za kitanzania za zaidi ya shilingi milioni 13,550,000/= pamoja na mtambo wa kutengeneza pesa bandia nyumbani kwa mmoja wao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kibaha mkoani Pwani Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo amesema mnamo tarehe 10 mwezi huu majira ya saa mchana huko kijiji cha Msata wilaya ya kipolisi Chalinze mkoani Pwani jeshi la polisi liliwakamata watu wanne wakiwa na pesa bandia za kitanzania noti 155 za tsh 10,000 zenye thamani ya shilingi 1550,000/= ambapo Mbaraka Miraji Fundi (48) Mzaramo na Zena Issa Naringa (42) mmakonde wote wakiwa ni wakazi wa Buza jijini Dar es Salaam walikamatwa.
Kamanda Lutumo alisema Kukamatwa kwa Watuhumiwa hao kulitokana na taarifa za raia mwema aliyeitilia mashaka noti ya Tsh.10,000/= aliyoipokea kama malipo ya huduma katika nyumba ya kulala wageni huko Msata.
Alisema baada ya mahojiano na watuhumiwa hao jeshi la Polisi mkoa wa Pwani lilifanikiwa kuwabaini washirika waoambao ni Masumbuko Paul Kiyogoma (54), muha mkazi wa Goba jijini Dar es salaam na Elias Silas Wandiba (50) Msukuma mkazi wa Kimara Suka jijini Dar es salaam wakiwa na pesa nyingine bandia zenye thamani ya shilingi 12,000,000/= zikiwa ni noti zenye thamani ya Tsh 10000/=, 5000/=, na 2000/=.
Aidha katika upekuezi kwenye makazi yao polisi walifanikiwa kukamata mtambo wa kutengeneza pesa hizo bandia na zana zingine kama vile computa, kemikali mbalimbali, gundi jiki, tina, rangi, visu na bunda la karatasi zikiwa katika hatua mbalimbali za kutengenezwa fedha bandia.
“Mtambo huo wa kutengeneza pesa bandia ulikamatwa katika makazi ya mmoja wa watuhumiwa huko Goba jijini Dar es salaam” alisema Kamanda Lutumo.
Hatahivyo Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani limetoa taadhali kwa wanannchi kuwa makini na fedha wanazopokea kutoka kwa watu wasiowafahamu ikiwa ni pamoja na wateja wao kwa kuzikagua na kuhakiki alama za fedha halali zinazokuwepo.
“Vilevile wahalifu wanaojihusisha na biashara hii haramu watambue wazi kuwa jeshi la Polisi kwa kushirikia na raia wema watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria” alisema Kamanda Lutumo.