Shilingi milioni 107 zimepatikana kwaajili ya kununua mbegu Bora za kilimo za kurudishia kilimo cha Wakulima ambao mashamba yao yaliathirika na mafuriko ya Mto Rufiji huko Wilayani Rufiji.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kupokea msaada wa vyakula na magodoro kutoka Huduma ya Arise and shine inayoongozwa na Mtume buludoza Boniface Mwamposa huko Ikwiriri Wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Amesema Waziri wa TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa binafsi ametoa shillingi milioni 50, wakazi wa Rufiji ambao wanaishi nje ya Wilaya ya Rufiji wametoa shilingi milioni 13. 7 na Wakuu wa mikoa 26 walizichanga na kuzikabidhi kwa Mheshimiwa Mchengerwa amekabidhi Mkuu huyo wa Wilaya shilingi milioni 44 na kufanya jumla ya shilingi milioni 107. 7 zitanunua mbegu kwaajili ya wakulima hao.
“Tayari tumeshaanza kufanya mchakato kupitia Maafisa Kilimo wanaohusika kwaajili ya kufanya manunuzi ya mbegu ilitupate mbegu zitakazowatosheleza wakulima wetu” alisema Meja Gowele.
“Lakini vile vile wizara ya kilimo imeshafanya tathimini ya kuwekeza kupata mbegu kwaajili ya kuwasaidia Wananchi pindi maji yatakapopungua waendelee na kushughulika na shughuli zao za kilimo”
Akizungumzia ugawaji wa viwanja vya makazi mapya ya Waathirika hao katika eneo la Kata ya Chumbi na Muhoro Meje Gowele alisema Wakala wa misitu Tanzania TFS Wilaya ya Rufiji imetoka maeneo ya viwanja 600 ili Wananchi hao wapate makazi ili wasirudi tena kuishi mabondeni isipokuwa huko mabondeni watumie kwa Kilimo tu.
Alisema viwanja hivyo 600 vimekwishapimwa hivyo amesema kwasasa wanawahamasisha wale maeneo yao yalikubwa na mafuriko na ambao wapo kwenye maeneo hatarishi waende kuamia katika maeneo ya viwanja vilivyoandaliwa na serikali ambako ni salama zaidi.
Aliongeza kuwa viwanja vingine vinaendelea kuandaliwa katika eneo la kijiji cha Chumbi ambako Wataalamu wa idara ya ardhi wanaendelea na mchakato wa kulipima ilikupata viwanja vya kutosha kwaajili ya Waathirika hao wa mafuriko ya Mto Rufiji ambao walipata changamoto ya makazi kwenye maeneo ya mabondeni ili waamie huko wasirudi mabondeni.
Meja Gowele alisema Waathirika hao wa mafuriko kwasasa wanaishi kwenye kambi ya muda kwaajili ya kuwahifadhi kipindi hiki cha dharula ya mafuriko sio Kambi ya kudumu na baada ya muda kambi hiyo itafungwa.
“Wapo ambao wanaondoka kwa utaratibu ambao ndugu zao wanawahitaji kuwachukua ndugu zao wanaenda kwa ndugu zao wanapewa chakula cha kwenda kuanzia kujikimu maisha wanaenda kwa ndugu zao walikuwa 496 mpaka sasa wamebaki 311 ambapo walioondoka walioondoka kwa hiyari yao ambao sawa na Kata 82 ambapo mwanzoni kulikuwa na kaya 117” alisema Meja Gowele.
“Hasa wale ambao ndugu zao wamekubali kuwachukua na wale ambao wamepata mahali pa kwenda kwani tuliwachukua kwa dharula hawakujua pakwenda Wala hawakujua pakufikia tunawaruhusu kuondoka”
Meja Gowele alisema maji yameanza kupungua katika Mto Rufiji ingawa bado utabili wa hali ya hewa unaonyesha bado mvua zitaendelea kunyesha hivyo bado anaendelea kutoa tafadhali na kuwashawishi Wananchi wasirudi mabondeni kwenye maeneo waliyotoka bali wakae kwenye maeneo salama.
“Hata katika Hali ya Kawaida hatuhitaji watu wakae hatarishi wakae maeneo salama” alisema Meja Gowele.
Aidha alishukuru kwa msaada huo wa kutoka Huduma ya Arise and shine inayoongozwa na Mtume Boniface Mwamposa na kuahidi kusimamia kuwafikishia walengwa.
Mtume Mwamposa aliwalishwa na Mchungaji Emmanuel Sanga alisema wameleta magodoro 50 na mifuko 150 ya unga wa uzito kilo 10.