NA. MWANDISHI WETU
Viongozi katika Mikoa na Halmashauri nchini, wametakiwa kuweka jitihada za kujiandaa kuzuia na kukabiliana na maafa hususan katika kipindi hiki cha mvua ambazo zimeanza kunyesha nchini.
Maagizo hayo yametolewa Novemba 22, 2023 Mjini Mtwara na Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga wakati wa ufunguzi wa kikao kazi na ziara ya kukagua utekelezaji wa hatua zinazochukuliwa kuzuia na kujiandaa kukabiliana na maafa kwa kamati ya usimamizi wa maafa mkoa wa Mtwara.
Naibu Waziri amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kukumbushana wajibu muhimu wa kila mmoja kuwajibika katika eneo lake ili kuokoa maisha na kulinda mali za wananchi.
“Kikao kazi cha leo kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa”
“Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea”
“Tunapongeza mikoa na halmashauri kwa kuchukua hatua za mapema kutekeleza maelekezo haya, Ofisi ya Waziri Mkuu imepokea taarifa na mipango iliyowasilishwa kuhusu namna ambavyo mnachukua hatua katika maeneo yenu katika kuzuia na kukabiliana na kupunguza madhara yanayoweza kusababisha na mvua zinazoendelea” amesisitiza Naibu Waziri
Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, ameipongeza ofisi ya Waziri Mkuu kwa juhudi ambazo imekuwa ikizifanya katika kuikinga jamii na maafa.
“Tunayo furaha sana kwa uzinduzi wa kikao hiki, sisi kama Mtwara ni moja ya mikoa wenye shughuli nyingi za uwekezaji kupitia mkakati wetu wa kuifungua Mtwara, sasa shughuli hizi huwa zinaweza kupelekea mabadiliko ya kimazingira na kusababisha majanga mbalimbali”
“Kwa hiyo nasisitiza kamati zote zitakazohusika katika mafunzo haya kuhakikisha kuwa zinazingatia yote yatakayofundishwa kwa ajili ya kuja kuyafanyia kazi na kuzikinga jamii zetu na majanga mbalimbali” amesema Kanali Abbas
=MWISHO=