Na.Mwandishi wetu-IRINGA
Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),tarehe 14 Septemba 2022 imefanya ziara ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha mkoani Iringa kujionea athari za uvamizi wa mifugo katika eneo la Bonde la Ihefu . Katika ziara hiyo, Bodi ilishuhudia takribani mifugo zaidi ya laki Mbili ikiwa ndani ya hifadhi.
Awali, akiwasilisha taarifa ya Hifadhi kwa Bodi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Meing’ataki alibainisha kwamba operesheni iliyofanyika kwa siku mbili ilifanikiwa kukamata mifugo zaidi ya elfu moja na mia tisa katika eneo hilo la Ihefu na itaendelea kwa siku 10 zaidi kuanzia tarehe 13 septemba 2022 hadi tarehe 23 septemba 2022.
Akipokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya TANAPA,
Jenerali (Mstaafu) George Waitara alisema “ leo tumejionea uvamizi mkubwa wa mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha. Ikumbukwe hifadhi hizi ni mali yetu sote watanzania na ni sehemu ya uchumi wa Tanzania, wakati mifugo ni mali ya mtu mmoja mmoja. Hivyo ni jukumu letu kulinda hifadhi ambayo ni ya Watanzania wote kwa faida ya sasa na ya baadaye”
Aidha, Jenerali Waitara aliongeza kuwa mifugo itakuwa chanzo cha kufa kwa hifadhi zetu, kwani inaua mifumo ya Ikolojia na kuhatarisha kutoweka kwa wanyama na mimea. Hivyo ni muhimu hifadhi hizi zikalindwa kufa na kupona.
Naye Prof. Wineaster Anderson ambae ni mmoja wa wajumbe wa Bodi hiyo, alisema TANAPA ina wajibu mkubwa wa kulinda maliasili zilizomo hifadhini kwa faida ya Watanzania wote.
“Tuna wajibu mkubwa katika Taifa hili wa kulinda maliasili hizi pamoja na miradi ya kimkakati kama Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere ambalo linategemea maji kutoka vyanzo vilivyomo hifadhini Ruaha. Kiasi kikubwa cha fedha kimekwishatumika kujenga bwawa hilo na wananchi wana mategemeo makubwa ya kunufaika nalo.
Hivyo sisi tukishindwa kulinda hivi vyanzo vya maji tutadaiwa na Watanzania sio tu leo, bali hata baada ya maisha yetu hapa duniani” aliongeza Profesa Wineaster.
Kwa upande wake Mjumbe mwingine wa Bodi, Kamishna wa Polisi Nsato Marijani, alisisitiza kuongeza nguvu katika kufanya doria na kuendeleza operesheni ya kuwaondoa wavamizi wote katika eneo la hifadhi hiyo.
Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema aliishukuru Bodi ya Wadhamini kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha kujionea changamoto kubwa ya uvamizi wa mifugo ambayo ni tishio kwa uhifadhi nchini.
Alibainisha kuwa endapo hapatakua na juhudi madhubuti na za dhati za kudhibiti mifugo, itapelekea kufa kwa hifadhi zetu ambazo ni tunu kwa Taifa, na zimekuwa zikituletea fedha, sifa na fahari ndani na nje ya nchi yetu.