Home Kitaifa MIAKA MITATU YA RAIS DKT SAMIA UCHUMI WA NCHI WAIMARIKA KWA KUKUA...

MIAKA MITATU YA RAIS DKT SAMIA UCHUMI WA NCHI WAIMARIKA KWA KUKUA KWA ASILIMIA 5.2

Na Magrethy Katengu

Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kwa kukuwa kwa asilimia 5.2 kufuatia kuporomoka kutoka asilimia 7 hadi asilimia 4.2 mwaka 2020 ikiwa ni madhara ya mlipuko wa UVIKO-19 duniani, vita za Urusi dhidi ya Ukraine sambamba na mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati.

Akielezea mafanikio hayo kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema ukuaji huo umeifanya Tanzania kusalia katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati ikimaanisha pato la wastani la kila mwananchi kwa mwaka (GNI per capital) ambapo ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080, lakini mwaka 2022 ni dola 1,200.

Serikali pia imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo kwa sasa ni chini ya 4% – kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),” ameeleza katika taarifa yake.

Vile vile, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa toshelezi ambapo katika kipindi chote cha miaka mitatu hadi Desemba 2023, nchi ilikuwa na akiba inayotosha kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa miezi 4.5, ikiwa ni kiwango cha juu ya lengo la miezi 4. Akiba hiyo ni sawa na dola za Marekani bilioni 5.4.

Akizungumzia Wizara ya Madini amesema katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi 2021 hadi Februari 2024 Wizara ya Madini imefanikiwa kuiendeleza sekta kwa namna mbalimbali ikiwemo kukusanya maduhuli yatokanayo na ada mbalimbali, mirabaha, faini na penati na kufikisha kiasi cha shilingi trilioni 1.93.

Awali mwaka 2021/22 ilikuwa shilingi bilioni 591.5 lakini hadi kufikia mwaka 2023/24 imefikia shilingi bilioni 690.4,” amesema Matinyi.
Aidha Matinyi amebainisha kuwa, katika kipindi cha Machi 2021 hadi Februari 2022 mauzo ya madini mbalimbali yalikuwa shilingi bilioni 157.34 lakini kufikia kipindi cha Machi 2023 hadi Februari 2024 mauzo yamefikia shilingi bilioni 476.8.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!