Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha inakamilisha haraka barabara ya mchepuko katika eneo la Mlima wa Inyala Kijiji cha Shamwengo mkoani Mbeya ili kupunguza matukio ya ajali yanayojitokeza mara kwa mara katika eneo hilo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipotembelea eneo la Inyala mahali zilipotokea ajali mbili hivi karibuni ka kusababisha vifo vya watu wapatao 25. Amesema Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 2.5 inapaswa kujengwa kiwango cha lami haraka kama suluhisho la muda mfupi litakarorahisisha upishanaji wa magari katika eneo hilo na kukabiliana na changamoto za ajali za mara kwa mara.
Halikadhali Makamu wa Rais amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Urich Matei kuhakikisha anasimamia ukaguzi wa magari yanayopita katika eneo la mlima wa Inyala ili kuepusha madhara ya ajali zinazojitokeza kutokana na ubovu wa magari hayo.
Aidha Makamu wa Rais ametoa siku kumi kwa Tanroads Mkoa wa Mbeya kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa miundombinu ya ukaguzi wa magari inayoendelea kujengwa katika eneo hilo ambalo linakabiliwa na changamoto za ajali mara kwa mara.
Makamu wa Rais amesema serikali inasikitishwa na madhara ya ajali yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali na kuwataka wahusika wakiwemo jeshi la polisi kutimiza wajibu wao kwa kuchukua hatua za kudhibiti ajali hizo zinazogharimu Maisha ya watu. Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo upanuzi wa barabara inayopita mkoani Mbeya kuanzia Igawa hadi Tunduma mkoani Songwe.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewasalimu wananchi wa Kijiji cha Shamwengo kilichopo kata ya Inyala ambapo amesema serikali itakamilisha ujenzi wa Zahanati ya Kijiji hicho ulioanza kujengwa na wananchi kwa kutoa shilingi milioni 100 za umaliziaji pamoja na kuchimba kisima katika eneo hilo ili kusaidia upatikanaji wa huduma za maji.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi hao kwa jitihada zao za kuanzisha mradi huo pamoja na moyo wao wa kujitolea katika kusaidia majeruhi wa ajali zinazotokea katika eneo hilo