Na Lusungu Helela- Arusha
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Ridhiwani Kikwete amesema matumizi ya mfumo wa PIPIMS, PEPMIS na HR Assessment katika Utumishi wa Umma nchini itaimarisha Utumishi wa Umma kwa kuwabana Watumishi wanaopenda kukaa ofisini pasipo kufanya kazi.
Mhe.Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jijini Arusha wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Chuo cha Ufundi Arusha ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kukagua mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma na Taasisi (PEPMIS na PIPMIS) na Mfumo Maalum wa Tathmini ya hali ya Rasilimaliwatu Serikalini (HR Assessment).
Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Utumishi wa Umma kwa kuhimiza uwajibikaji ili kuhakikisha kama Taifa linakuwa na utumishi wa umma unaopimika kwa kumpima Mtumishi mmoja mmoja pamoja na Taasisi kwa ujumla.
Ameongeza kuwa mfumo wa PEPMIS umekuja kuwa mbadala wa OPRAS ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anayelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji inayowezesha viongozi na watumishi wa umma kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakati na mahali popote.
Katika hatua nyingine Mhe. Kikwete amewataka Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala kuacha kukaa ofisini badala yake waende maeneo ya kazi ili kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi walio chini yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe.John Mongela amesema zama hizi hazihitaji watu wenye misuli kutokana na kukua na teknolojia. Hivyo, teknolojia imerahisisha utendaji kazi na sisi tuko tayari kuisimamia utekelezaji wake.
Amesema ujio wa mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala wataanza kubadilika na kuachana na utaratibu wa kizamani wa utendaji kazi wao.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuiomba Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora kuwanoa upya Maafisa Utumishi na Maafisa Utawala wa mikoa na Halmashauri kwani utendaji wao wa kazi sio wa kuridhisha ikizingatiwa wao ndo wenye jukumu la kuwasimamia watumishi wengine.