Home Kitaifa MHE. KAPINGA: TANZANIA KUFAIDIKA NA UZOEFU WA SAUDI ARABIA KATIKA MAFUTA NA...

MHE. KAPINGA: TANZANIA KUFAIDIKA NA UZOEFU WA SAUDI ARABIA KATIKA MAFUTA NA GESI

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia katika kuimarisha Sekta ya Nishati, hususan katika Mafuta na Gesi, Nishati Safi ya Kupikia, na Nishati Jadidifu.

Mhe. Kapinga amesema hayo wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhandisi Mohammed Albrahim, katika mji wa Riyadh tarehe 19 Desemba 2024, nchini Saudi Arabia.

Amesema kuwa, Tanzania imekuwa ikishirikiana na nchi hiyo kwa muda mrefu katika biashara ya mafuta na maeneo mengine ya maendeleo. Hivyo, mahusiano hayo yanaendelea kuimarika zaidi kwa kuwa mahitaji ya nishati yanazidi kuongezeka, na uwekezaji zaidi unahitajika katika kuendeleza Sekta ya Nishati, ikiwemo Mafuta na Gesi Asilia, Nishati Jadidifu, na Nishati Safi ya Kupikia.

Mahusiano ya Tanzania na Saudi Arabia katika Sekta ya Nishati ni ya muda mrefu. Nchi hizi mbili zimekuwa na lengo la kuboresha ushirikiano wao katika kuendeleza sekta ya nishati,” amesema Kapinga.

Aidha, ameeleza kuwa Tanzania, kama nchi inayoendelea, inahitaji kuimarisha zaidi miundombinu yake ya nishati kwa ajili ya maendeleo. Hivyo, imekuwa ikishirikiana na nchi zenye uzoefu mkubwa katika sekta hizo ili kupata matokeo chanya, kwa kuwa nishati ni msingi mkuu wa maendeleo.

Amesema Saudi Arabia imekuwa ikijulikana kwa uwezo wake mkubwa katika uzalishaji wa mafuta na gesi, na imekuwa ikiwekeza katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo Afrika Mashariki. Kwa upande wa Tanzania, yenye rasilimali za Gesi Asilia na viashiria vya uwepo wa mafuta, inapata uzoefu, ujuzi, na teknolojia kutoka Saudi Arabia katika kuchimba, kusafisha, na kusafirisha mafuta na gesi pamoja na kuimarisha miundombinu ya rasilimali hizo.

Vilevile, Mhe. Kapinga amesema kuwa kuimarika kwa Sekta ya Nishati nchini kutaiwezesha Tanzania kusambaza umeme utakaozalishwa nchini kwa nchi jirani ambazo zimeonyesha nia ya kuhitaji nishati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Mhandisi Mohammed Albrahim, amesema kuwa nchi yake inajipanga kuwekeza zaidi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, utunzaji wa mazingira, na kuwekeza zaidi katika Sekta ya Mafuta na Gesi, Nishati Jadidifu, na Nishati Safi ya Kupikia.

Amesema, pamoja na kwamba wamegundua mafuta mengi, wanajipanga kuendana na sera za kidunia kwa kuwekeza katika Nishati Safi ambayo inahifadhi mazingira.

Ameongeza kuwa, Saudi Arabia inatambua juhudi zinazofanywa na Tanzania kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa kinara katika kutekeleza ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!