Home Kitaifa MHE. KAIRUKI AZINDUA KAMATI YA KITAIFA YA KUONGOA SHOROBA, AIPA MAELEKEZO MAHUSUSI.

MHE. KAIRUKI AZINDUA KAMATI YA KITAIFA YA KUONGOA SHOROBA, AIPA MAELEKEZO MAHUSUSI.

Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amezindua Kamati ya Kitaifa ya kuongoa shoroba za Wanyama pori katika kongamano la kwanza la kitaifa la kujadili usimamizi madhubuti wa shoroba hizo ili kuleta manufaa ya kiuchumi huku akiielekeza kamati hiyo kufanya kazi kwa kasi zaidi.

Katika hotuba yake aliyoitoa leo Desemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha wadau zaidi ya mia mbili, Mhe. Kairuki amesisitiza kuwa katika usimamizi huo Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali ili kufikia azma hiyo kwa kuwa jambo hilo haliwezi kutekelezwa na Wizara peke yake na amewaomba wadau wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kushirikiana na serikali.

Amesema sambamba na zoezi hilo Serikali itaendelea kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya shoruba ili maeneo hayo yaweze kutumika kikamilifu katika mawanda mengine kama utalii wa picha hivyo kuinufaisha jamii inayozunguka maeneo hayo nan chi kwa ujumla wake.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa matumizi bora ya ardhi pia yatasaidia kuainisha maeneo yatakayotumika kwa ajili ya huduma za kijamii kama shule hospitali, kilimo na malisho.

Lakini kuwa na mpango wa mtumizi bora ya ardhi haitoshio tumeendelea kusisitiza Halmashauri zetu za wilaya na vijiji kupitia serikali za mitaa pamoja na wenzetu kutoa elimu wa umma ili waweze kujua vijiji gani vimeshaandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi lakini pili kulinda yale matumizi yaliyoainishwa ili yafuatwe” amesisitiza Mhe. Kairuki

Amefafanua kuwa pia lengo la kikao cha Kwanza cha jukwwa la kitaifa la kuongoa shoroba ni kujadili suala la kuhifadhi shoroba za wanyamapori nchini ili kutekeleza Mpango wa Kuongoa na Kusimamia Shoroba 20 za Wanyamapori za Kipaumbele nchini – 2022-2026, (Tanzania Wildlife Corridors Assessment, Prioritization and Action Plan).

Kikao hiki kinafanyika kwa mara ya kwanza na kimepewa jina National Corridor Forum kikilenga pamoja na mambo mengine kuwaleta pamoja wadau wa uhifadhi kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kujadili utekelezaji wa Mpango wa Kuongoa na Kusimamia Shoroba 20 kati ya 61 za Kipaumbele nchini (2022-2026) – (Tanzania Wildlife Corridors Assessment, Prioritization and Action Plan)” amesisitiza Mhe. kairuki

Ameyataja malengo mengine ya kikao hicho kuwa ni pamoja na kuainisha wadau na kuweka maazimio ya nani afanye nini na wapi ili kuongoa na kuhifadhi shoroba za wanyamapori, hasa zilizo hatarini, Serikali kutoa kauli thabiti kwa wananchi kuhusu tafsiri ya maeneo ya shoroba za wanyamapori kuwa sio hifadhi na zitaendelea kuwa katika ardhi za vijiji; na kutoa kauli juu ya fursa mbalimbali zilizopo kwenye shoroba hizo, hasa utalii na biashara ya hewa ukaa ili wananchi waweze kuzitumia na kunufaika na rasilimali za wanyamapori.

Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya kuoingoa Shoroba, Linnah Kitosi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais amesisitiza kuwa jambo la kwanza kwa sasa ni kuwaelimisha wananchi waweze kuzitambua shoroba ili wanyama waendelee kupita na wananchi waweze kufanya shughuli zao bila kuleta migongano na madhara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!