Na John Mapepele.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaaa na michezo. Mhe Pauline Gekul leo Julai 8,2022 amezindua Kamati maalum ya kuratibu mjadala wa namna bora ya kusimamia hakimiliki nchini.
Katika uzinduzi huo ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Saidi Yakubu.
Akizindua Kamati hiyo kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Pauline Gekul ameitaka kamati hiyo kufanya kazi kwa weledi ili kukidhi matarajio ya wasanii na haki zao ambapo amesema Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewaamini wajumbe wa kamati hiyo kuwa watakwenda kufanya kazi hiyo kikamilifu.
“Serikali imefanya maamuzi ya Kuunda Kamati hii ya Kitaifa yenye mchanganyiko wa wadau mbalimbali muhimu kwenye tasnia kwa niaba ya wadau wengine kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wadau hasa wa Sekta ya Sanaa nchini kuhusiana na namna mirabaha inavyokusanywa na kugawanywa, kuwepo kwa vitendo vya uharamia katika kazi zao na elimu duni kwa wadau kuhusu masuala hayo, kamati hii inatarajiwa kuratibu mjadala wa namna bora zaidi ya kusimamia Hakimiliki nchini” amefafanua Mhe. Gekul.
Amezitaja Hadidu za Rejea za kamati hiyo kuwa ni pamoja na kupendekeza mifumo bora zaidi ya kukusanya na kugawa mirabahainayoshabihiana na mifumo inayotumika kwingineko duniani, kupendekeza njia bora zaidi za kupambana na uharamia, kupendekeza mfumo bora zaidi wa uendeshaji wa Taasisi ya Hakimiliki, kupendekeza masuala mengine muhimu ya usimamizi wa Hakimiliki nchini.
Mhe. Gekul ameongeza majukumu mengine ya Kamati hiyo kuwa ni pamoja na kuratibu Kikao cha Wadau wa Hakimiliki kujadili mapendekezo ya Kamati, na Kuwasilisha Taarifa ya Kamati kwa Mhe. Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Aidha amesema kuna mpango kazi ambao Ofisi ya Hakimiliki ilishaandaa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu kuanzia mwaka huu wa fedha, ambapo inatarajiwa mapendekezo ya Kamati yatakapokuwa tayari yatawasilishwa Wizarani ili yaweze kuingizwa kwenye mpango kazi wa Taasisi ili kuwa na namna bora zaidi ya kusimamia hakimiliki nchini.
Kamati hiyo inaundwa na Victor Michael Tesha, Mwenyekiti wa Kamati, Mtaalamu wa Fedha na Masoki, Dkt Saudin Mwakaje, Makamu Mwenyekiti wa Kamati, Mtaalamu wa Hakimiliki na masuala ya miliki Ubunifu, Dkt. Asha Salum Mshana, Mkurugenzi Msaidizi Haki za Wasanii, Bw. Nimesh S. Mawji, Katibu wa Kamati,Mtaalamu wa Sheria ya Miliki Bunifu.
Wajumbe wa Kamati hiyo ni pamoja na Mhe. Hamis Mwinjuma, Mbunge wa Muheza na Msanii Mkongwe, Dkt. Omary Mohamed, Kamishna wa Utamaduni Zanzibar, Bw. Paul Mattysse, Mzalishaji wa Muziki, Bi. Safina Kimbokota, Msanii wa Sanaa za Ufundi, Bw. Torriano Salamba, Mdau wa Hakimiliki Mitandaoni, Bw. Gabriel Kitua, Mwenyekiti Chama cha Wachapishaji na Bw. Twiza Mbarouk, Katibu Mkuu Shirikisho la Filamu Tanzania.