Home Biashara MHE. DKT. ASHATU KIJAJI AMEWAASA WAMILIKI WA VIWANDA KUONGEZA NGUVU NA KASI...

MHE. DKT. ASHATU KIJAJI AMEWAASA WAMILIKI WA VIWANDA KUONGEZA NGUVU NA KASI YA KUZALISHA BIDHAA KATIKA MNYORORO MZIMA WA THAMANI

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amewaasa wamiliki wa viwanda kuongeza nguvu na kasi ya kuzalisha bidhaa katika mnyororo mzima wa thamani kama mbolea, sukari, mafuta ya kula na ngano ili kukidhi mahitaji ya ndani, kuuza nje ya nchi, kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo nje ya nchi na kujitosheleza hata wakati wa changamoto kama COVID 19 na vita vya Urusi na Ukraine.

Waziri Kijaji ameyasema hayo Julai 14, 2022 katika Mkutano na Wanachama wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) katika ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam. Mkutano huo ulilenga kujadiliana mambo ya kipaumbele kwa maendeleo ya Sekta ya Viwanda katika ukuaji wa uchumi wa nchini.

Aidha, Waziri Kijaji amewashauri Wanachama wa Shirikisho hilo kizalisha kiushindani bidhaa zenye ubora na viwango vinavyotakiwa ili ziweze kuingia katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika pamoja (AfCFTA) na Dunia kwa ujumla ili kutimiza lengo la Serikali la kuifanya Tanzania kuwa lango la biashara Afrika.

Dkt. Kijaji pia amesema Wizara itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za viwandani pamoja na Sekta Binafsi katika kuendeleza Sekta ya viwanda nchini inayotegemewa kuongeza thamani malighafi, kuongeza ajira, pato la taifa, kuongeza fedha za kigeni na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) Bw. Paul Makanza ameishukuru Serikali kwa hatua mbalimbali iliyozichukua kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara ikiwemo marekebisho ya Sheria, kuanzisha mifumo mbalimbali ya kutoa huduma kielektroniki, kufuta ada na tozo pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya barabara, umeme, reli ya kisasa na diplomasia ya kiuchumi.

Pamoja na hayo Bw. Makanza ameiomba Serikali kutekeleza Mpango huo wa Maboresho kwa haraka, kulinda maboresho yaliyofanyika kwa kuzingatia kutokuanzisha ada au kodi mpya itakayokuwa kero pamoja na kulinda bidhaa zinazozalishwa nchini huku ikisimamia ushindani wa biashara wa haki pamoja na kupunguza ushuru wa malighafi za mafuta ya kula ili kuongeza uzalishaji na kuuza mafuta hayo kwa bei rahisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!