Home Biashara MHE. CHANDE AIPONGEZA MKOMBOZI PLC BENKI KWA KUPANDA DARAJA LA SOKO LA...

MHE. CHANDE AIPONGEZA MKOMBOZI PLC BENKI KWA KUPANDA DARAJA LA SOKO LA UJASIRIAMALI – EGM

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, amezitaka kampuni na taasisi za fedha zilizo kwenye daraja la Soko la Ujasiriamali (EGM) kuweka mikakati madhubuti ya kukua ili waweze kufikia viwango vya juu vya utendaji vinavyotakiwa na Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS).

Mhe. Chande ameyasema hayo wakati wa kutangazwa rasmi kupandishwa daraja kwa usajili wa Benki ya Biashara ya Mkombozi (MKCB) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage House, Jijini Dar es Salaam

Alisema kuwa hatua hiyo ni matokeo ya jitihada, nidhamu pamoja na ushirikiano wa wafanyakazi na uongozi wa kuweka nguvu pamoja ya kufikia malengo.

“Ni dhahiri kuwa hatua hii ni matokeo ya juhudi kubwa, nidhamu na ushirikiano wa karibu kati ya uongozi wa benki, wafanyakazi, wawekezaji na mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha.

Kupitia juhudi zenu, mmeweza kuleta ufanisi na kukidhi vigezo vya kupandishwa daraja katika Soko la Hisa la Dar es salaam. mmeonyesha kuwa taasisi za kifedha za ndani zinaweza kukua, kujisimamia na kuhimili ushindani,” aliongeza Mhe. Chande.

Aliioongeza MKCB Kwa kuwa taasisi ya kwanza kabisa kuhamishwa kutoka daraja la EGM hadi daraja la MIMS katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Hili ni tukio la kihistoria la Benki kupanda daraja la usajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam kutoka soko la kijasiriamali kwenda soko kuu la uwekezaji, na imeingia katika vitabu vya historia” alisistiza Mhe. Chande.

Mhe. Chande alibainisha kuwa kupandishwa daraja kwa Benki ya Biashara Mkombozi kwenda soko kuu la uwekezaji ni uthibitisho kuwa Soko la Hisa la Dar es Salaam linakua na lina uwezo wa kuvutia na kuendeleza kampuni zinazoweza kushindana katika ngazi za juu.

Alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi na kuwa mafanikio hayo ya MKCB ni kielelezo tosha cha uwezekano na fursa zilizopo katika soko la hisa.

Mafanikio hayo yanatupa matumaini na ari ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuziwezesha kampuni nyingine kufuata nyayo hizo na kuongeza mipango na sera za kuendeleza na kuimarisha soko la mitaji zinaendelea kuzaa matunda” alisema Mhe. Chande

Aidha, alisema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha mazingira ya uwekezaji ya aboreshe a zaidi, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, sera na kanuni za biashara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MKCB, Bw. Respige Kimati alisema kuwa jumla ya mali za Benki zimeongezeka kutoka Sh. bilioni 64 Disemba mwaka 2013 hadi sh. bilioni 255.8 kufikia Disemba 2023.

Aidha, alisema kumekuwa na ukuaji mkubwa katika mikopo inayotolewa na Benki hiyo kutoka bilioni 28.8 Disemba 2013 hadi sh. bilioni 134.3 Disemba 2023.

Kiwango hiki ni sawa na wastani wa ukuaji wa asilimia 36.6 kwa mwaka, ukuaji ambao unathibitisha azma yetu ya kusaidia biashara za sekta binafsi, taasisi na biashara za ngazi mbalimbali ili kusaidia kutekeleza malengo yao ya kibiashara na utoaji wa huduma,” alisema Bw Kimati.

Alisema kuwa MKCB iliongeza amana kutoka sh bilioni 49.7 Disemba 2013 hadi sh bilioni 207.4 Disemba 2023, sawa na wastani wa ukuaji wa asilimia 32 kwa mwaka.

Bw. Kimati alisema mwelekeo wa faida umekuwa ukiongezeka, kutoka sh. milioni 342.7 Disemba 2013) hadi sh. bilioni 8.6 Disemba 2023, ikiwa ni kiwango cha wastani cha ukuaji wa asilimia 240 kwa mwaka.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa Benki yao imewekeza katika mifumo ya kidijitali ili kuwezesha utoaji wa huduma za kidijitali kulingana na maendeleo ya kiteknolojia katika tasnia ya huduma za benki.

MKCB ina matawi 13 katika miji ya Moshi, Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Morogoro, Dodoma, Bukoba, Iringa, na Njombe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!