Home Kitaifa MHANDISI NDOLEZI PETRO AMETANGAZA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE WA KIGOMA KUSINI

MHANDISI NDOLEZI PETRO AMETANGAZA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE WA KIGOMA KUSINI

Waziri Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu-Bunge, Sera, Vijana, Kazi na Ajira wa ACT Wazalendo, Mhandisi Ndolezi Petro, ametangaza nia rasmi ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini. Tangazo hili alilitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 16 Januari, 2024, katika Kijiji cha Nguruka, Kata ya Nguruka, jimboni humo, ambapo alizungumzia changamoto zinazokikumba jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara, ukosefu wa pembejeo za kilimo, migogoro ya ardhi, na changamoto za huduma za afya kwenye vituo vya afya.

Mhandisi Ndolezi amesisitiza kuwa msukumo wake wa kugombea umetokana na hali ngumu wanayokutana nayo wananchi wa Kigoma Kusini. Alieleza kuwa atatoa sera na mipango yake kwa kina wakati wa kampeni akipata ridhaa ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Aidha, Mhandisi Ndolezi ni mtetezi wa ajenda za vijana na amekuwa mstari wa mbele katika kupigania maslahi yao kupitia majukwaa mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kujenga uchumi unaozalisha ajira nyingi ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana. Anapigia pia chapuo uwepo wa mifuko ya hifadhi ya jamii jumuishi, ili kuwanufaisha hata wale walio katika sekta isiyo rasmi, ambao ni asilimia 91 ya nguvu kazi ya Taifa.

Hii ni baada ya Chama cha ACT Wazalendo kufungua milango rasmi kwa watia nia kugombea nafasi za Urais, Ubunge, na Udiwani kupitia Katibu Mkuu wa Chama hicho, Ndugu Ado Sahibu, tarehe 15 Januari, 2025. Kwa upande wa Urais, hadi sasa, wawili wameonyesha nia; Ndugu Dorothy Semu, ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, na Ndugu Othman Masoud Othman Sharif, ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!