Home Kitaifa MGORE MIRAJI ATOA MCHANGO WA NG’OMBE WANA JAMII YA MUSOMA KUKUTANA LEO...

MGORE MIRAJI ATOA MCHANGO WA NG’OMBE WANA JAMII YA MUSOMA KUKUTANA LEO JIONI

Na Shomari Binda – Musoma

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi Taifa, Mgore Miraji, ametoa mchango wa ng’ombe kwa ajili ya kitoweo kwa wana jamii ya Musoma watakapo kutana leo jioni.

Umoja wa jamii ya watu wa Musoma unakutana leo, Februari 21, kwenye ukumbi wa Mwenbeni Complex kuanzia saa 1 usiku, ikiwa ni fursa ya kujumuika, kufahamiana, na kujadili masuala mbalimbali ya kijamii na maendeleo.

Mweka Hazina wa umoja huo, Ismail Massaro, amesema kuwa wamepokea mchango huo wa ng’ombe kutoka kwa Mgore, ambaye ni mmoja wa wana jamii, na maandalizi ya chakula yanaendelea vizuri.

Massaro alieleza shukrani kwa mchango huo ambao umekuwa sehemu muhimu ya kuandaa hafla hiyo, ambayo inatarajiwa kuwakutanisha watu wengi.

Alisema, “Suala la kutoa ili kukutanisha watu ni jambo jema. Kilichofanywa na Mgore ni muhimu kuigwa na kila mwenye nafasi.”

“Tunamshukuru dada yetu kwa kutuahidi kutupatia ng’ombe kwa ajili ya kitoweo katika hafla yetu ya leo, na ametekeleza ahadi yake. Maandalizi mengine yote yanaendelea vizuri, na kikubwa tunawaomba wana umoja kufika kwa wakati kwenye ukumbi wa Mwenbeni Complex na kushiriki kwa pamoja,” aliongeza Massaro.

Katika hafla hiyo ya jamii ya Wana Musoma, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, pamoja na wageni mbalimbali.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!