Na Shomari Binda-Musoma
MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza la Wazazi Taifa Mgore Miraji ameichangia kiasi cha shilingi laki 5 timu ya Bweri FC. Timu hiyo ndio mabingwa wa soka Mkoa wa Mara msimu wa 2023/2024 wanajiandaa na ushiriki wa ligi ya mabingwa wa mikoa itakayoanza machi 8.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi kiasi hicho cha fedha Mgore amesema timu hiyo ni wawakilishi wa mkoa hivyo kila mmoja anapaswa kuisaidia.
Amesema kwenda jijini Mwanza kwenye kituo walichopangiwa kunahitajika fedha ili waweze kushiriki kwa ufanisi.
Mgore amesema yeye kama mpenda michezo anaipongeza timu hiyo kwa kuchukua ubingwa wa mkoa na ataendelea kuwa karibu nayo.
“Najua timu inayo mahitaji mengi inapokwenda kushiriki ligi tuichangie ikafanye vizuri na iingie ligi daraja la pili”
“Kila mmoja aguswe na Bweri FC na aweze kuichangia kwa kuwa ndio wawakilishi pekee wa mkoa kwenye ligi ya mabingwa” amesema Mgore.
Amesema iwapo timu hiyo itafanya vizuri na kuingia ligi daraja la pili itaongeza idadi ya timu kwenye ligi za Tanzania.
Katika ligi ya mabingwa wa mkoa timu ya Bweri FC imepangwa kituo cha Mwanza pamoja na mabingwa wengine kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita na Kagera.