Na Shomari Binda-Musoma
MJUMBE wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Mgore Miraji amechangia mifuko 20 ya saruji na “treep 10” za mawe ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Musoma mjini.
Akitamka mchango huo agosti 20 kwenye kikao cha baraza la jumuiya hiyo ngazi ya Wilaya amesema katibu kama mtendaji anapaswa kuwa na makazi bora ili aweze kutekeleza majukumu yake.
Amesema kama kiongozi ndani ya jumuiya ya wazazi ameona kuanza kuchangia ujenzi ili uweze kujengwa msingi na kukamilisha nyumba hiyo.
Mgore amesema katika ziara aliyoifanya pamoja na viongozi wengine wa kitaifa mikoani ameona kasi ya ujenzi wa nyumba za watumishi na kutamani kasi hiyo kufanyika kwenye wilaya ya Musoma na mkoa wa Mara.
” Kama kiongozi nimeona kasi ya ujenzi wa nyumba za watumishi natoa mifuko 20 ya saruji na mawe ili kasi hiyo ionekane nyumba ya Katibu Wilaya ya Musoma.
” Nipongeze kikao kizuri cha baraza na licha ya mchango wangu kwenye ujenzi wa nyumba ya Katibu nna zawadi ya t.shert nimewaletea kama sare ya jumuiya yetu”,amesema.
Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa Mgore amewakumbusha wajumbe wa baraza hilo kufanya uhamasishaji kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na lile la makazi.
Amesema uchaguzi unaanzia kwenye uandikishaji hivyo uhamasishaji lazima ufanyike na ni moja ya majukumu ya jumuiya ya wazazi.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi ya CCM wilaya ya Musoma mjini Eras James ameshukuru mchango wa kiongozi huyo kwenye ujenzi wa nyumba ya Katibu.
Amesema kutokana na mchango wake huo ndani ya jumuiya wameamua kumpa hati ya pongezi pamoja na viongozi wengine wanao changia kwenye jumuiya hiyo.