Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Bi. Fatma Mbarouk amesema ni muhimu kuwa na mfumo utakaosaidia kuangalia Utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na changamoto zinajitokeza kwenye utekelezaji huo ili kuweka mikakati ya kuzitatua kwa lengo la kuhakikisha matarajio ya AfCFTA yanafikiwa.
Ameyasema hayo Juni 18,2024 wakati akifungua Mkutano Maalum wa Maafisa Wakuu wa Biashara (STOs) kuhusu Mfumo wa Mapitio ya Utekelezaji wa AfCFTA (AFIRM) unaofanyika kuanzia Juni 18 – 22, 2024 ukifuatiwa na ngazi Ya Mawaziri Juni 24 – 25, 2024 Zanzibar Tanzania
Aidha amebainisha kuwa Mkutano huo umelenga kupitia na kukubaliana Andiko la Kitaalam kuhusu utaratibu wa mapitio ya utekelezaji wa AfCTFA (AFIRM) lililotokana na Mikutano ya Makatibu Wakuu iliyofanyika Kigali – Rwanda, Arusha – Tanzania na Abuja – Nigeria
”Napenda pia kuchukua nafasi hii kuwakaribisha hapa Zanzibar na kwenye huu Mkutano wetu maalum kwa ajili ya kuangalia kwa kina Mfumo wa mapitio ya utekelezaji wa AfCTFA. Nina imani kuwa ni Mkutano huu ni muhimu sana kwetu na Afrika kwa ujumla. Nina imani tutakuwa na mjadala mzuri na tutaweza kukubaliana kwa pamoja.” Amesema Bi. Mbarouk.
Kikao hicho muhimu kimejumuisha Maafisa Wakuu wa Biashara (STOs) kutoka nchi wanachama wa AfCFTA na Jumuiya za Kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Kati (ECCAS), Shirika la Kikanda la Maendeleo kati ya Serikali (IGAD), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), Jumuiya ya Nchi za Sahel-Sahara (CEN-SAD,) Tume ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA), Umoja wa nchi za Kiarabu wa Maghreb (UMA) na Benki ya Uagizaji na Usafirishaji nje Bidhaa za Afrika (AFREXIMBANK)