Home Kitaifa MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA (EHMS) WAIONGEZEA UFANISI HOSPITALI YA AMANA.

MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA (EHMS) WAIONGEZEA UFANISI HOSPITALI YA AMANA.

Katika kuongeza ubora wa ufanisi wa utendaji kazi na udhibiti mapato hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam -AMANA imefunga mfumo maalum wa kielektroniki(EHMS) ambao kwa kiasi kikubwa umeboresha huduma hospitalini hapo.

Akizungumza na Mwandishi wetu, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt.Bryceson Kiwelu amesema mfumo huo umefungwa toka mwaka 2012 ili kuhuisha huduma za hospitali.

“Mfumo huu umefungwa toka mwaka 2012 chini ya uongozi uliokuwepo na mwaka 2014 mfumo ulianza kutumika rasmi hapa hospitali” alisema Dkt. Kiwelu.

Aidha Dkt.Kiwelu amesema sababu kubwa za kufunga kwa mfumo huo wa (EHMS),ni kwamba kulikuwa na kazi ngumu sana ya kutunza kumbukumbu kwenye nakala ngumu na pia ugumu wa kufanya tafiti kutokana na miandiko ya baadhi ya madaktari kutosema vizuri na pia nakala hizo hazidumu kwa muda mrefu.

Pia Dkt.Kiwelu amesema kwa sasa mfumo huo umesaidia sana huduma za hospitalini hapo kwa kusimamia mapato na pia taarifa zinafika Serikalini kwa haraka na sahihi kwa wakati unaotakiwa.

Kwa upande wa matibabu Dkt.Kiwelu amesema mfumo wa (EHMS) umesaidia sana kugundua kwa haraka magonjwa ambayo sio ya kawaida hali ambayo inawasaidia kuchukua hatua kwa haraka au kuwasiliana na taasisi nyingine kwa wakati, pia umerahisisha kujua mahitaji ya bidhaa dawa na vifaa tiba kwani kwa wiki,mwezi na kwa mwaka hali inayowafanya waweze kupanga bajeti yao kulingana na fedha iliyopo.

“Kwa sasa wagonjwa wote wanaofika katika Hospitali ya Amana wanapata mahitaji yao toshelezi kwa dawa zile zinazohitaji kwa huduma husika na imetusaidia kujua kama tuna upungufu wa dawa ya aina gani ili tuweze kuongeza” alisema Dkt.Kiwelu.

Akiendelea kuelezea mfumo huo wa (EHMS) mganga mfawidhi huyo wa hospitali ya Amana amesema umesadia kujua maeneo gani yanatakiwa kuweka kipaumbele kuwa na madaktari bingwa kulingana na mahitaji ya jamii husika,ambapo kwa sasa wana madaktari bingwa 29.

Kwa upande wa mapato ya Hospitali Dkt.Kiwelu amesema awali Kabla hawajaanza kutumia mfumo huo wa kidigitali mapato yalikuwa wastani wa shilingi bilioni 2.6 kwa mwaka,tofauti na sasa baada ya kufunga mfumo wa (EHMS) mapato yameongezeka na kufikia wastani wa shilingi bilioni 4.5 kwa mwaka mmoja wa fedha, hali iliyopelekea kuboresha miundombinu ya hospitali na kuboresha huduma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!