Na Scolastica Msewa, Rufiji.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele amefungua miradi miwili ya Barabara na mradi wa maji kwenye zahanati iliyoshindwa kufikiwa na Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2024 huko makao makuu ya wilaya ya Rufiji akimuwakilisha Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava ambaye alitakiwa kuufungua mradi huo Mei 5, mwaka huu msafara wa Mwenge ulishindwa kufika kutokana na Barabara ya Utete Nyamwage kufurika maji.
Tukio hilo la baraka la ufunguzi wa miradi hiyo ni baada ya Mwenge wa Uhuru kushindwa kufika katika eneo hilo May 5, mwaka huu kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na maji kujaa na kuchimba barabara ambapo Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 alitoa maelekezo kwa DC Gowele kuufungua mradi kwa niaba yake baada ya kuukagua kwa picha jongefu (video) na Nyaraka na kuupitisha ufunguliwe.
Kwa Upande wa Mradi wa maji kwenye zahanatii, zoezi lilifanyika katika zahanati ya Nyandakatundu katika Kitongoji cha Nyandakatundu Kata ya Chemchem wenye thamani ya shilingi milioni 7.9 ambao unatarajiwa kuhudumia Wananchi 1,119 wa Kitongoji hicho,
Mradi mwingine ni Mradi wa barabara ya kiwango cha lami katika mji mdogo wa Utete wenye thamani ya shilingi milioni 504.9 ikiwa ni fedha kutoka serikali kuu kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini TARURA ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 100.
Meja Gowele aliwataka madereva kufuata sheria za barabarani ili kupunguza ajali za mara kwa mara.
Gowele aliwataka wakazi wa eneo hilo kuutunza na kuulinda miradi hiyo ili uendelee kutoa huduma kwa Wananchi.
Uzinduzi huo umefanyika na kushuhudiwa na Kamati za Ulinzi na usalama za Wilaya ya Rufiji, Wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na serikali.
Mradi huo ni miongozi mwa miradi 7, iliyotakiwa kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu.