Na Ritha Jacob – Ruvuma
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Bara, Issiaka Mchinjita, ametoa wito kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kumtafutia wakala wa mbegu eneo maalum la kulima mbegu zake ili kuwaachia wananchi mashamba yao. Hatua hiyo itawezesha wakulima kuzalisha mazao yanayotumika kulisha Watanzania.
Mchinjita alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, alipokuwa akiendelea na ziara yake ya kutembelea mikoa sita, iliyoanza Julai 22, 2024. Ziara hiyo ina lengo la kusajili wanachama milioni 10 kwa miezi 10 na kusikiliza wananchi.
“Waziri Bashe ameanzisha mashamba ya BBT kule Dodoma, ni vyema akaelekeza wakulima wa mbegu huko badala ya kuwafukuza wananchi na wakulima kutoka mashamba yao. Kama serikali ina ardhi ya kutosha kiasi cha kuwahimiza vijana wote waliokosa ajira kuenda kulima, kwa nini wakulima wanatolewa kwenye mashamba yao?” alisema Mchinjita.
Aidha, aliongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa uzalishaji wa makaa ya mawe, ambayo yanapelekwa kwenye mikoa mingine yenye viwanda. Mkoa huo hauna viwanda ambavyo vingesaidia kuzalisha malighafi zinazopatikana hapo, hatua ambayo ingewasaidia wananchi kupata vipato na vijana kupata ajira.
Mchinjita pia alizungumzia kuhusu mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 600 kwa kutumia makaa ya mawe, ambao haujaendelea. Alisema mradi huo ungeweza kuchochea uwekezaji kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati na hivyo kuvutia wawekezaji kutoka duniani kote kuwekeza katika malighafi zinazopatikana Ruvuma.