OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Mkurugenzi wa Halmashauri atakayeshindwa kusimamia Mradi wa Uboreshaji wa miundombinu ya Miji ya Tanzania(TACTIC) atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo leo Septemba 23, 2023 kwenye hafla ya kushuhudia utiaji saini Mkataba wa Mradi huo iliyofanyika jijini Dar es salaam.
“Wakurugenzi mna tabia za kukaa na fedha kwenye akaunti bila kutekeleza miradi wengine walikaa nazo mpaka nilivyokuja huku nikasema nitawachukulia hatua ndio wakaanza kukimbizana kutekeleza miradi sasa kwa yeyote atakayekaa na fedha za mradi huu na kuchelewa kuanza utekelezaji wa mradi wa TACTIC nitamchukulia hatua za kinidhamu,” ameonya.
Amesema Mradi huo ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na serikali ya kuboresha miundombinu ya Barabara, mifereji ya maji ya mvua, stendi za mabasi, masoko, pamoja utunzaji wa Mazingira katika maeneo ya mijini.
“Lengo kuu la mradi wa TACTIC ni kuboresha usimamizi wa ukuaji wa Miji pamoja na kuziwezesha Halmashauri za Miji na Majiji kutoa huduma bora kwa wananchi, mikataba inayosainiwa leo ni sehemu ya miradi itakayotekelezwa kwa Mkopo wa Benki ya Dunia utakaogharimu kiasi cha Dola za Marekani Milioni 410 sawa na Sh.Trilioni moja na inatekelezwa katika Miji 45 nchini,” amesema.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni kwa awamu tatu na katika Kundi la kwanza linahusisha Miji 12 ambayo ni Mwanza CC, Mbeya CC, Arusha CC, Dodoma CC, Ilemela MC, Morogoro MC, Kahama MC, Kigoma Ujiji MC, Songea MC, Sumbawanga MC, Tabora MC na Geita TC ambapo utekelezaji wake unaanza mwaka huu wa Fedha 2023/24.
Katika kundi la Pili, itahusisha Miji 15 ya Tanga CC, Moshi MC, Kibaha TC, Iringa MC, Bukoba MC, Singida MC, Bariadi TC, Shinyanga MC, Musoma MC, Lindi MC, Mpanda MC, Njombe TC, Mtwara Mikindani MC, Babati TC and Njombe TC na utekelezaji wake utaanza mwaka ujao wa Fedha 2024/25.
“Katika kundi la tatu Miji 18 itahusika ambayo ni Kasulu TC, Tunduma TC, Vwawa TC, Ifakara TC, Makambako TC, Masasi TC, Nanyamba TC, Handeni TC, Bagamoyo DC, Mafinga TC, Tarime TC, Chato DC, Bunda TC, Mbinga TC, Mbulu TC, Nzega TC, Kondoa TC and Newala TC ambayo utekelezaji wake utaanza mwaka ujao wa Fedha 2024/25.
Naye, Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, Adolf Nduguru amesema mikataba ya ujenzi wa barabara na mitaro inayosainiwa leo katika kundi hilo la kwanza itagharimu Sh. Bilioni 276.18 kwa Miji yote 12 na gharama za usimamizi zitakuwa sh. Bilioni 17.05.
Awali, Mratibu wa mradi huo, Mhandisi Hamprey Kanyenye amesema katika mikataba inayosainiwa leo zitajengwa barabara zenye urefu wa kilometa 147.54 kwa kiwango cha lami nzito, madaraja, vivuko maji, uwekaji wa taa za barabarani zenye kutumia mfumo wa umeme jua, njia za watembea kwa miguu, mitaro ya maji ya mvua kwa pande zote za barabara na mitaro mikubwa ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 24.66 itajengwa.