Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa, leo April 26, 2023, Mlele, Mpanda, mkoani Katavi, amefunga mafunzo ya askari 231 wa Jeshi la Uhifadhi akisema ajira hizo zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, sasa zinakwenda kusaidia kuwatatulia wananchi kero ya wanyama wakali wakiwemo tembo katika baadhi ya maeneo nchini.
“Leo mmefuzu hapa Taifa linawasubiri mkatoe mchango wenu na hapa hapa naagiza moja kwa moja mpangwe kwa dharura kusaidia kutatua kero ya tembo na wanyama wengine wakali katika baadhi ya maeneo mbalimbali nchini,” aliagiza Waziri Mchengerwa akishangiliwa na wahitimu hao ambao walionekana kuiva na kuwa tayari kwa kazi hiyo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi, akimwalika Mhe. Waziri alitoa taarifa kuwa wahitimu wote hao leo leo watapewa barua zao za kuripoti katika vituo mbalimbali vya uhifadhi nchini tayari kuanza safari yao ya utumishi wa umma kwani Serikali ya Rais Samia ni ya kazi na kazo inapaswa iendelee.