NA Shomari Binda-Butiama
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo ametoa ekari 204 kwaajili ya makazi na kilimo.
Ekari hizo amezitoa kwa wananchi wa Kitongoji cha Mtukura Kijiji cha Sirorisimba wilayani Butiama kwenye eneo lake la uwekezaji.
Akizungumza na wananchi wa Kitongoji hicho na viongozi wa wilaya ya Butiama wakiwemo wa idara ya ardhi amesema ametoa ekari hizo ili kusaidia jamii.
Amesema eneo alilolitoa kwa wananchi limo ndani ya eneo la uwekezaji analolimiliki na kulipia serikalini na kufanyia shughuli za kilimo na ufugaji.
Mathayo amesema wananchi wanapaswa kulitumia eneo hilo kwaajili ya makazi na shughuli za kilimo ili kujiwezesha kiuchumi.
“Nimetoa sehemu ya eneo la uwekezaji ili kusaidiana na jamii tulitumie eneo hilo na tukae kwa utulivu tukishirikiana kwa pamoja” ,amesema Mathayo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mtukura Maswi Magweiga amesema wanamshukuru muwekeaji Vesastus Mathayo kwa kuwa na moyo wa huruma na kutoa eneo analolimiliki kwa wananchi.
Amesema wapo watu wanaomiliki maeneo na hawajawahi kuyatoa kwa wananchi lakini yeye amefanya hivyo.
Katibu wa Tarafa ya Kiagata Levina Marwa amesema wananchi waliokabidhiwa eneo hilo wanapaswa kuwa na vyoo kwenye makazi yao na kupeleka watoto shule.