Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini, Vedastus Mathayo ametoa kiasi cha shilingi milioni 3 na laki 4 kusaidia ujenzi wa ofisi ya CCM Kata ya Mshikamano na wajasiliamali wa soko la Saa Nane.
Mchango huo ameutoa leo alipokuwa akifatilia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwenye Kata hiyo kabla ya kufanya mkutano wa hadhara.
Mathayo ambaye yupo kwenye muendelezo wa mikutano ya hadhara kwenye Kata 16 za jimbo hilo amesema uhai wa chama unahitajika na ofisi ni sehemu ya hamasa.
Amesema katika kuona ofisi ya chama inakamilika ameanza kwa kutoa kiasi cha shilingi milioni 2 na laki 4 na ataendelea kuchangia hadi kukamilika kwake.
Akizungumza na viongozi wa CCM Kata ya Mshikamano,amesema kazi za chama zinapaswa kufanyika sehemu nzuri na atahakikisha ofisi hiyo inakamilika.
“Ndugu zangu viongozi nimeanza kwa kuchangia kiasi hicho cha fedha kwaajili ya ofisi yetu na tutaendelea kuchangia hadi itakapokamilika” amesema Mathayo
Akiwa katika soko la Saa Nane lililopo Kata hiyo,mbunge Mathayo amewachangia wajasiliamali wa dagaa na mbogamboga kiasi cha shilingi milioni 1 ili kuongezea mitaji.
Kwenye mkutano wa hadhara,Mathayo amewaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa kuwa ameendelea kutoa fedha nyingi jimbo la Musoma mjini.
Amesema kwenye sekta ya elimu,afya,maji na miundombinu fedha nyingi zimetolewa na wananchi suala la michango hasa kwenye madarasa wamepumzishwa.