Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa viti maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete amewahimiza wanawake kujitokeza kugombea nafasi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadae mwaka huu.
Licha ya kutakiwa kujitokeza kuomba nafasi hizo za uongozi kwenye uchaguzi huo lakini pia wametakiwa kushiriki kwenye uboreshaji wa daftari la wapiga kura ili waweze kuchagua na kuchaguliwa.
Kauli hiyo ameitoa leo juni 21 mwaka huu wakati akifungua kongamano la 3 la Ushirika wa Mama wa Kikristo wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara (UMAKI).
Amesema wanawake wanayo nafasi kubwa ya kuongoza na uchaguzi unaokuja wasibaki nyuma na wajitokeze kuomba nafasi.
Ghati amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha njia ya mwanamke kuongoza vyema hivyo hawapaswi kubaki nyuma katika kuomba nafasi.
Amesema wanapokuwa mstari wa mbele kwenye masuala ya Mungu na imani kwenye uongozi wa kijamii wanapaswa kujitokeza
“Niwashukuru sana mama zangu kwa kunialika kuwa mgeni rasmi kwenye kongamano hili ambalo masuala ya kiimani yanazungumzwa na yale ya kijamii, mimi nimetokana na nyie lakini tunakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani tujitokeze kugombea lakini pia tushiriki kwenye uboreshaji wa daftari la wapiga kura” amesema
Aidha amewaomba kina mama hao wa kikristo kusimama kupinga matukio ya ukatili yanayotokea kwenye jamii yakiwemo ya watoto.
Mwenyekiti wa Ushirika wa Mama na Mtoto Dayosisi ya Mara mchungaji Martha Henry amesema kongamano hilo litakalofanyika kwa siku 3 litazungumzia kuwajenga wanawake kiimani na masuala ya kijamii.
Amesema kwenye masuala ya kijmii watazungumzia namna wanawake wanavyoweza kushiriki kupambana na masuala ya ukatili wa kijinsia.
Katika ufunguzi huo mbunge huyo wa viti maalum ameongoza harambee na kupata kiasi cha shilingi milioni 6 pamoja na sufulia kubwa 2 kuwawezesha wanawake hao.