Na Shomari Binda- Musoma
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Mara Ghati Chomete ameitumia siku ya kumbukumbu ya miaka 24 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuichangia viti 50 jumuiya ya wazazi Musoma vijijini.
Hiyo ni ahadi aliyoitoa kwa jumuiya hiyo hivi karibuni katika kuisaidia kuweza kukaa kwenye vikao na mradi wa jumuiya.
Akizungumza wakati wa kukabidhi viti hivyo kwa niaba ya mbunge Ghati Chomete diwani wa Kata ya Mwigobero Manispaa ya Musoma Mariam Sospeter amesema ahadi za mbunge huyo ni zenye kutekelezeka.
Amesema mbunge Ghati aliahidi na ameitumia siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kutekeleza ahadi yake aliyoitoa kusaidia viti kwenye jumuiya hiyo.
Mariam amesema mbunge huyo wa viti maalum mkoa wa Mara amekuwa na utaratibu wa kufika kila wilaya na pale kunapokuwa na changamoto kwenye chama cha mapinduzi na jumuiya zake amekuwa akichangia.
” Mbunge mheshimiwa Ghati yupo kwenye majukumu mengine na ameniomba nije nitekeleze ahadi yake aliyoitoa kwenye jumuiya ya wazazi Musoma vijijini”
“Aliahidi kutoa viti 50 kwaajili ya vikao na mradi wenu na leo nimekuja kuvikabidhi kwa niaba yake”, amesema Mariam.
Akipokea mchango huo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Musoma vijijini Jackson Nyakia amempongeza mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi yake.
Amesema mbunge Ghati Chomete ni kiongozi muungwana na akiahidi anatekeleza na ndicho alichokifanya.
Nyakia amesema wanamshukuru kwa mchango wake wa viti 50 alivyowachangia ambavyo wamekabidhiwa na diwani Mariam.