Home Kitaifa Mbaroni kwa tuhuma za kughushi vyeti vya leseni ya Udereva

Mbaroni kwa tuhuma za kughushi vyeti vya leseni ya Udereva

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watano wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa ya kughushi vyeti vya udereva pamoja na wizi wa mitandaoni.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa alisema Julai 25 mwaka huu walifanikiwa kumkamanta Esau Yakobo(26) Mkazi wa Mecco Kaskazini Wilaya ya Ilemela kwa kughushi vyeti na leseni za udereva.

Katika vyeti hivyo vingi vikiwa na majina na namba pamoja na vivuli mbalimbali vya leseni za udereva ,picha mabalimbali za ‘Pasport size’ ambazo hutolewa na Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(veta) pamoja na barua mbalimbali za kutoka Jeshi la Polisi.

Kamanda alisema katika barua hizo zipo ambazo zimeghushiwa saini ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza kimakosa kisheria.

“Tulimkamata baada ya kumkuta kwa John Msemo (45), Ofisa Mauzo wa Kampuni ya Chrolide Exide aliye fika kituo cha Polisi Mwanza kwa ajili ya uhakiki wa madaraja ya leseni yake na barua iliyoghusiwa saini Julai 5 Mwaka huu.” alisema

Kamanda Mutafungwa alisema katika zoezi linaloende la kuhakiki leseni za madereva pamoja na vyeti vya udereva, John Msemo alidai kupata vyeti hivyo kutoka kwa Sixmond George (48) ambaye ni Mkufunzi wa Chuo cha Udereva Nyanza na ni Mkazi wa Igoma baada ya kumpatia fedha.

Alisema mtuhumiwa mwengine ni Samwel Bose (47) Mwalimu wa Chuo cha Udereva Chanila na ni Mkazi wa Ibanda juu ambaye naye amekutwa na barua ya kughushi iliyohusu uhakiki wa leseni kutoka kwa Jeshi la Polisi ambazo wamekuwa wakizitumia kujinufaisha kwa kuwaadaa wananchi.

“Tumefanikiwa kumkamata Mtandao wa wahalifu hawa na vifaa walivyokuwa wakivitumia kughushi nyaraka ikiwemo Printer moja aina ya Epson,Computer aina ya HP na Flash mbili.” alisema Kamanda Mutafungwa

Pia Kamanda alisema Julai 27 mwaka huu walifanikiwa kumkamata Abdulahim Karungila(41)Mkazi wa Mtaa wa Rwazi Kata ya Kahororo Bukoba Mjini pamoja na Heri Kabuya (36) Mkazi wa Mtaa wa Kyaya Kata ya Kahororo kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kiharifu mitanadoni.

Kamanda alisema watuhumiwa hao walikutwa na nyaaraka za watumishi na wastaafu wa Serikali zikiwa katika mfumo wa machapisho mbalimbali pamoja na line mbalimbali za simu.

Watuhumiwa hao walikuwa wakiwapigia simu watumishi wa serikali na kuwatajia kumbukumbu zao za daftari la utumishi huku wakiwataka watume fedha ili wawarekebishie kumbukumbu zao za utumishi.” alisema

Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa alisema mnamo Julai 25 mwaka huu muda wa saa moja na nusu usiku katika kijiji cha Ntundu Kata ya Busangi Wilaya ya Msalala Mkoa wa Shinyanga walifanikiwa kumkamata Prisca Clement(25)Mkazi wa Buhingo Wilaya ya Misungwi akiwa na mtoto wa mwaka mmoja na miezi 9 aliyeibiwa kutoka Zanzibar alikokuwa anafanya kazi za ndani.

Kamanda alisema mtoto huyo aliibiwa Julai 10 mwaka huu Visiwani Zanzibar baada ya mzazi wa mtoto huyo kumuachia Prisca Clement amuangalie wakati alipokwenda kwenye majukumu mengine ndipo mtuhumiwa alipata nafasi ya kutoroka.

“Alitoroka na mtoto huyo mpaka Mkoa wa Mwanza na baadae wakaenda na mtoto huyo hadi Mkoa wa Shinyanga,baada ya kuhojiwa alikiri kumuiba mtoto huyo kwa lengo la kwenda kumuuza.” alisema

Aliongeza kuwa tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza wamekwisha wasiliana na wazazi wa mtoto huyo na atakabidhiwa kwao baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!