Na Shomari Binda-Serengeti
MAWAZIRI 3 wa kisekta wamemaliza ziara yao ya siku 2 mkoani Mara kwa maagizo ya serikali kwa kutoa maelekezo kwa wananchi kuzingatia sheria za nchi wakati serikali ikiendelea kuwahudumia.
Mawaziri hao wamefika mkoani Mara kwa maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoyatoa hivi karibuni bungeni baada ya maombi ya mbunge wa Tarime vijijini Mwita Waitara kuomba serikali ifike kuona zoezi la uwekaji mipaka Hifadhi ya Serengeti lilivyofanyika.
Wakiwa wilayani Serengeti Kijiji cha Bisalala Kata ya Sedeco ,wamezungumza kwa nyakati tofauti na wananchi hao na kudai ili kuepukana na migogoro mbalimbali inapaswa sheria za nchi ziweze kufuatwa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Marry Masanja,amewataka wananchi kuacha kuingiza mifigo hifadhini kwaajili ya malisho kwani sheria inakataza na anayefanya hivyo hufikishwa Mahakamani.
Amesema wananchi wamekuwa wakilalamika kukamatiwa mifugo na kutozwa faini lakini jambo hilo lipo kisheria na ili kuepusha kulalamika wafuate sheria na kuzingatia maelekezo yanayotolewa.
“Wizara imesikia yale wananchi mliyoyaomba kufanyiwa ikiwa ni pamoja na kupatiwa miradi ya kimaendeleo tutaendelea kufanya lakini ni muhimu kuzingatia sheria za kulinda rasilimali za nchi”, amesema Masanja.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Angella Kairuki amesema serikali ya awamu ya 6 ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,inaendelea kufanya maendeleo kwa wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu,afya na miundombinu hivyo wananchi wanalaswa kuinga mkono.
Amesema katika sekta ya elimu kila mmoja anashuhudia kila pembe ya nchi ikiwemo Serengeti ujenzi wa madarasa ya kisasa ukiendelea na serikali imetoa fedha nyingi.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula,amesema kwa sasa migogoro ya ardhi inakwenda kuisha kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na malalamiko mengi yameshughulikiwa.
Amesema kwa sasa suala la upatikanaji wa hati kwa wananchi sio shida kwa kuwa zinawafuata walipo tofauti na miaka ya nyuma kuvuka mikoa kufatilia hati.
Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenarali Suleiman Mzee,amewataka wananchi kuwa na utaratibu mzuri wa kuwasikiliza viongozi wanaokuja kutatua kero zao na kuwapa mambo ambayo serikali itawatatulia.
Wananchi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Serengeti wameiomba serikali kuendelea kuwafikia kwa shughuli za maendeleo ikiwemo miradi ya maji.