Home Kitaifa MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI

Na Shomari Binda-Musoma

MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali mkoani Mara yametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na utu wa mtanzania.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Mara,Said Mtanda,wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Amesema mashirika hayo kwa mkoa wa Mara yamefanya kazi nzuri hususani ya kupambana na ukatili wa kijinsia na kustahili kupongezwa.

Mtanda amesema katika kuendelea kufanya majukumu yao ya kila siku ni kuhakikisha mashirika hayo yanafanya kazi kwa kuzingatia maadili mazuri ya mtanzania.

Amesema fedha zinazotolewa na wadau zisipelekee kufanya kazi kinyume na maadili ya mtanzania na kuvunja utu wa kibinadamu.

Mkuu huyo wa mkoa amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yanashirikiana vyema na serikali katika majukumu yao na kudai yupo tayari kuendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo.

Niyashukuru mashirika yote yasiyo ya kiserikali hapa mkoa wa Mara kwa kazi nzuri mnayoifanya hasa katika mapambano ya ukatili wa kijinsia.

Nimeambiwa yapo mashirika 286 na kati ya hayo 130 yapo kwenye hatari ya kufutwa kutokana na kutokulipa ada lakini wote nawapongezeni sana“,amesema Mtanda.

Mjumbe wa Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali( NACONGO)Robbi Samwel,ameyataka mashirika kuhakikisha yanalipa ada kwa mujibu wa taratibu ili kuepuka kufutwa na kutoa taarifa kwa wakati.

Amesema ulipaji wa ada ndio uhai wa shirika katika ufanyaji wa kazi na kuyataka kuzingatia suala hilo ili kuendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kwani ni asilimia chache ya mashirika yaliyolipa ada.

Katika mkutano huo maafisa maendeleo ya jamii kutoka wilaya za mkoa wa Mara wametoa taarifa za mashirika yaliyopo kwenye wilaya hizo na kazi wanazozifanya kwenye jamii zikiwemo za kupambana na ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa kampeni ya kitaifa ya kupambana na ukatili wa kijinsia (Smaujata) Joyce James,amemuomba mkuu wa mkoa kuwawezesha kuweza kuwa na uchumi utakaowawezesha kuifikia jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!