Home Michezo MARA MSIMU HUU TUNA JAMBO LETU LA KUIPANDISHA BIASHARA UNITED LIGI KUU...

MARA MSIMU HUU TUNA JAMBO LETU LA KUIPANDISHA BIASHARA UNITED LIGI KUU – DC CHIKOKA

Na Shomari Binda-Musoma

MKUU wa Wilaya ya Musoma Juma Chikoka amesema msimu huu mkoa wa Mara una jambo lake moja la kuhakikisha timu ya Biashara United inapanda ligi kuu msimu ujao.

Kauli hiyo ameitoa septemba 8 kwenye uwanja wa Karume mjini Musoma kwenye tamasha la kuwatambulisha wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo maarufu kama “Kichuri Day”.

Amesema baada ya kushindwa kupanda ligi kuu msimu uliopita sasa msimu huu jambo ni moja kuhakikisha lengo linatimia

Chikoka amesema kupanda kwa timu hiyo kutayokana na ushirikiano wa pamoja baina ya timu na wadau wote wa mkoa wa Mara.

Amesema imempendeza Rais Dkt. Samia kumleta Musoma na kuomba ushirikiano kwa wana Musoma na mkoa wa Mara kiujumla kuhakikisha Biashara United inapanda ligi kuu msimu ujao.

“Msimu huu jambo ni moja tu kuhakikisha Biashara United inapanda ligi kuu msimu ujao na hili litafanikiwa iwapo tutashirikiana kwa pamoja”

“Tukishirikiana kwa pamoja kuanzia mwanzo wa msimu hakuna jambo litakaloshindikana tutakwenda ligi kuu msimu ujao” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma mjini Magiri Benedict amesema Musoma imepata mtu sahihi anayependa michezo na burudani hivyo atasaidia timu hiyo kupanda ligi kuu msimu ujao.

Magiri amemuomba mkuu wa Wilaya ya Musoma kusaidia kupata wadhamini ili malengo ya timu hiyo kurejea ligi kuu yatimie.

Awali mjumbe wa bodi ya timu ya Biashara United Augustine Mgendi amemuomba DC Chikoka kufikisha salamu kwa mkuu wa mkoa Kanali Evans Mtambi na wadau wengine kusaidia malengo ya kuipandisha timu hiyo yaweze kutimia.

Katika tamasha hilo licha ya tukio la kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi ulichezwa mchezo wa kirafiki kati ya Biashara United na Pamba Jiji ambapo timu hizo zilitoshana nguvu kwa kutokufungana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!