Home Kitaifa Mamlaka za maji zatakiwa kuwa na Mpango wa Biashara

Mamlaka za maji zatakiwa kuwa na Mpango wa Biashara

Wakurugenzi wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira wanaofanya kazi bila kuwa na mpango wa biashara wamefahamishwa kuwa watajiondosha katika nafasi hizo baada ya siku 90.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa angalizo hilo wakati akifunga Siku ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA day) jijini Dar es salaam na kusisitiza mkurugenzi wa mamlaka ya maji itakayoshindwa kuwa na mpango wake wa biashara atakuwa amejiondosha katika nafasi yake baada ya siku tisini kuanzia Machi 21.

“Haiwezekani kuwepo katika biashara wakati hauna mpango wa biashara” Mhandisi Luhemeja amesema na kuongeza kuwa kwa mamlaka itakayohitaji usaidizi iwasiliane na EWURA ili kufanikisha mpango wa biashara.

Pamoja na hilo, ameelekeza mamlaka ambazo hazina Mkataba wa Huduma kwa Mteja zihakikishe zinakuwa na mkataba, pia kuhakikisha mamlaka zisizokuwa na Mpango wa Kupambana na Upotevu wa Maji zinakuwa na mpango huo ndani ya siku 90.

Mhandisi Luhemeja amesema mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi kama timu, na kuelekeza mamlaka ambazo hazijalipa Tozo ya EWURA kufanya hivyo kabla ya tarehe 1 Julai, 2023.

Amesisitiza ni muhimu kuwa na viwango vya utendaji kazi, na kuzipa mamlaka za maji muda wa mwaka mmoja kuweka juhudi ya kupata Ithibati, itakayosaidia kupunguza malalamiko na kuweka viwango vya kazi.

Pia, mamlaka zimetakiwa kutenga fedha za ndani ili kuweza kuongeza mtandao wa huduma ya majisafi kwa wananchi. Aidha, amewataka watendaji wa mamlaka hizo kuangalia fursa nafuu za huduma ya kuondosha majitaka ikiwamo teknolojia mbalimbali zinazowezekana katika mazingira ya nchi yetu.

Naye Katibu Mkuu mstaafu Mhandisi Bashir Mrindoko akiongea katika hafla hiyo amewataka watendaji katika sekta ya maji kuwa wakweli na wazi hususan katika changamoto mbalimbali za kazi, badala ya kuzunguka katika kusema ukweli wa hali halisi iliyopo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!