Taarifa za Wizara ya Maji zinaonesha hadi Aprili, 2024 mtandao wa majitaka nchini ulikuwa kilometa 1455.93 ikilingalishwa na kilometa 1416.9 za Aprili, 2023, idadi ya maunganisho katika mtandao, usafirishaji na kutibu majitaka umefikia kilometa 58,650 kutoka 56, 923 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.
Aidha, pia taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ya utendaji wa mamlaka hizo kwa mwaka 2022/23, inaonesha ni mamlaka 21 tu kati ya 85 sawa na asilimia 24.7 ndizo zenye miundombinu ya kutibu majitaka na tope kinyesi kwa kipindi hicho.
Katika hotuba ya Ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Usafi wa Mazingira ya Naibu waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko , Jijini Dodoma iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi ameipongeza EWURA kwa kuandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Usafi wa Mazingira na Topekinyesi unaolenga kujenga jamii yenye afya bora na mazingira salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Naipongeza EWURA kwa kuja na mwongozo huu wa Kiswahili ambao unalenga kuziongoza mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira kutoa huduma ya usimamizi wa tope kinyesi kwa wananchi walio nje ya mtandao wa majitaka.” Amesema Lukuvi
Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso
amezikumbusha Mamlaka za Maji nchini kuzingatia mwongozo huo ambao umeweka misingi,mipaka, wajibu na majukumu ya utoaji huduma za usimamizi wa tope kinyesi zinazofanywa na mamlaka hizo.
“Ni vyema mnyororo wa huduma za usafi wa mazingira kuanzia kukusanya, usafirishaji na matumizi ya tope kinyesi ukazingatiwa ili kulinda afya za wananchi,” Amesema
Awali Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, amesema kuwa tathmini na tafiti zilizofanywa toka karne ya 19, zilibainisha kuwa watu wanapokaa kwenye mazingira safi, afya zinakuwa imara na ni njia ya kujikinga na magonjwa mengi.
Mwongozo wa Usimamizi wa Usafi wa Mazingira na Topekinyesi unawalenga wadau kama mamlaka za serikali za mitaa, sekta binafsi zinazotoa huduma ya usafi wa mazingira kwenye maeneo yasiyo na mtandao wa majitaka, wizara zenye dhamana, RUWASA na NEMC.