Na Salim Bitchuka
Imeelezwa kuwa taarifa sahihi na Elimu sahihi kwa mama wajamzito zitasaidia kupunguza vifo ya kinamama vitokanavyo na uzazi.
Hayo yameelezwa leo na Dkt. Maiko Masasi kutoka kituo cha Afya Round Table Mbagala jijini Dar es Salaam wakati walipotembelewa na uongozi wa Kampuni ya Hatua Group Afrika inayosimamia program ya Busela yenye lengo la kuhamasisha uwepo wa Afya bora kwa mama wajawazito hapa nchini.
Dkt. Maiko Masasi amesema ameguswa na kazi inayofanywa na Busela kwa kutoa elimu ya lishe, Mazoezi na elimu ya saikolojia, kitendo alichosema kitawezesha mama wengi wajawazito kujitambua wakiwa kwenye hali hiyo.
Aidha Daktari huyo kutoka kituo cha Afya Round Table Mbagala ametanabaisha kuwa anaamini taarifa sahihi zitawezesha wakinamama wajawazito kupata huduma zilizo sahihi,lishe iliyo bora huku akiweka wazi kuwa wimbi kubwa la kinamama wajawazito wamekuwa na upungufu wa damu wakati wa kujifungua kitendo kinachotokana na kukosekana kwa elimu ya kutosha ya lishe .
Kwa upande wake Afisa Manunuzi ambaye pia ni muelimishaji kutoka Busela Elly Julius amesema endapo mama mjamzito ataandaliwa mapema kwa kufanya aina ya mazoezi,lishe bora pamoja na kutayarishwa kisaikolojia kuna uwezekano mkubwa wa mama mjamzito kujifungua salama .
Kampuni ya Hatua Group Afrika kupitia programu yake ya Busela imekuwa ikitoa elimu ya Afya ya uzazi na Mazoezi kwa mama wajawazito kwa kuwafuata katika vituo vyao vya Afya na nyumbani na kutoa vifaa vya kujifungulia kwa mama wajawazito ambao wapo karibu kujifugua lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.