Wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Forodha, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda ametuma salamu kwa wote wanaojihusisha na uingizaji wa Mali za magendo kuwa zitataifishwa.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo tarehe 26.01.2025 katika maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Forodha Kamishna Mkuu Mwenda amesema Idara ya Forodha ipo madhibuti kupambana na uingizaji wa mali za magendo nchini kwa kuweka udhibiti Bandarini, kwenye viwanja vya ndege na mipakani.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema mali yoyote ya magendo itakayokamatwa ikiingizwa nchini itataifishwa na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo vinavyodhoofisha uchumi wa nchi.
Amesema katika kwa mwaka 2025 Tanzania inaadhimisha siku ya Kimataifa ya Forodha wakati ikiwa na mfumo wa Forodha wa TANCIS ulioboreshwa ambao utafanya kazi Bandarini, kwenye viwanja vya ndege na mipakani kwa ufanisi zaidi na kupunguza huduma za watu kuonana huku akili Mnemba ikihusika kwa kiwango kikubwa.
Amesema mfumo wa TANCIS ulioboreshwa ni tiba ya matatizo yote ya kiforodha kwenye uondoshaji shehena bandarini, mipakani na kwenye viwanja vya ndege ambapo jumla ya Taasisi 36 zimeunganishwa na mfumo huo.
Amesema, mfumo huo unapunguza muda wa kuondosha mizigo bandarini, jambo ambalo litasababisha biashara kufanyika kwa haraka na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Akiuzungumzia mfumo huo, Rais wa Chama cha mawakala wa forodha Tanzania, (TAFFA), Edward Urio, ameeleza matumaini yao kuhusu kuimarishwa kwa TANCIS, na kusifu uwezo wake wa kuboresha ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa mapato.
“Tunaamini mfumo huo utaongeza uwazi na ufanisi unakwenda kuwa tiba ya matatizo yote ya kiforodha kwenye uondoshaji shehena bandarini, mipakani na kwenye viwanja vya ndege,” amesema Urio.
Naye Kamishna wa Forodha Bw. Juma Bakari amesema mfumo mpya wa TANCIS umeimarika zaidi ya ule wa awali ulioanzishwa mwaka 2014 hivyo tija yake ni kubwa na utarahisisha ufanyaji wa biashara katika uingizaji na utoaji wa bidhaa nchini.
Amesema kutakuwa na matumizi bora ya taarifa, kwani takwimu zitawekwa kwa utaratibu, kusaidia maafisa wa forodha na taasisi nyingine katika kufanya uamuzi sahihi.
Kauli mbiu ya siku ya Forodha ni “Forodha itatekeleza dhamira yake ya usalama na ustawi”
Mwisho