Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Iramba imetoa semina ya siku moja kuhusu elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa kwa makundi ya watu wenye mahitaji maalum.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Januari 27, 2025, katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Katibu Tawala wa Wilaya ya Iramba, Bupe Mwakibete, amewataka wawakilishi hao kutoka vyama vya watu wenye mahitaji maalum waendelee kutoa elimu kwa wenzao juu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Aidha, Mwakibete amesisitiza kuwa jukumu la kupambana na rushwa ni la kila mtu, hivyo ni muhimu kushirikiana wakati wowote inapohitajika.
“Jukumu la mapambano dhidi ya rushwa ni letu sote. Tuhakikishe tunakuwa mstari wa mbele katika kupinga vitendo vya rushwa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi,” alisema Mwakibete.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania, Nassoro Ernest Amos, ameishukuru TAKUKURU kwa kutoa mafunzo hayo kuhusu elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa makundi ya watu wenye mahitaji maalum.
Aidha, amesema kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa.
“Tumepata elimu itakayotuwezesha sisi, watu wenye mahitaji maalum, kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa. Rushwa ni adui mkubwa wa haki, na wajibu wetu ni kuhakikisha tunachagua viongozi waadilifu wasiopatikana kwa njia za rushwa,” alisisitiza Nassoro Amos.
Mafunzo hayo yalihusisha baadhi ya wawakilishi kutoka Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), Chama cha Watu Wasioona (TLB), Chama cha Walemavu wa Viungo (CHAWATA), na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA).