Na Mercy Maimu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi, wataalamu na wawekezaji kujadili kwa pamoja namna bora ya kutunza, kusimamia na kuwekeza katika rasilimali adhimu za fukwe zilizopo nchini ili kuongeza mchango wake kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 23 Novemba 2022 wakati akifungua Jukwaa la Nane la Maendeleo Endelevu lenye dhima ya Usimamizi Madhubuti wa Fukwe kwa Maendeleo endelevu linalofanyika Jijini Mwanza.
Amesema unahitajika ubunifu katika kutumia zaidi ya kilomita 1400 za ukanda wa Pwani ya bahari na fukwe safi, hifadhi 3 za baharini,maeneo tengefu ya baharini 15, maziwa na mito mikubwa ambayo kwa pamoja inaongeza idadi kubwa ya fukwe ambazo bado hazijaweza kutumika kikamilifu kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Aidha Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita imeweka mkazo katika kuendeleza Uchumi wa Buluu pamoja na suala la hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Ameongeza kwamba dhamira ya Serikali ni kuharakisha maendeleo endelevu ya taifa kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 inayolenga kufikia uchumi jumushi wa Taifa lenye kipato cha kati na maisha bora kwa kila Mtanzania. Vilevile, Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano pamoja na mikakati mingine ya kisekta na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) vyote vimelenga kuiwezesha sekta binafsi kuwa kichocheo cha kukuza uchumi wa Taifa na kuleta maendeleo kwa watanzania.Pia ameagiza kila Mkoa, kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, pamoja na wadau wengine kujipanga na kuharakisha mchakato wa kuandaa mpango mkakati utakaoainisha namna ya kufanya uwekezaji wa kuendeleza fukwe zilizopo nchini pamoja na bustani za kupumzikia.
Amesema mchanganyiko mzuri wa uhifadhi ukiambatana na huduma za kitalii, utaleta hamasa katika kuongeza utalii wa ndani na nje katika maeneo mbalimbali ya nchini. Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa mikoa kutekeleza suala la upandaji miti kwa ufanisi ikiwemo ufuatiliaji wa miti hiyo kuhakikisha inafanikiwa kukua kama ilivyopangwa.
Pia amewaagiza kuweka malengo yanayotekelezeka ikiwemo kuwatumia wakala wa misitu nchini (TFS) katika elimu sahihi ya miti itakatokuwa rafiki wa vyanzo vya maji na mazingira.Awali akitoa taarifa za kuhusu kongamano hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) Kadari Singo amesema kongamano limelenga kujadili fursa zilizopo katika uwekezaji wa fukwe kama kichochezi cha maendeleo, changamoto zinazohusiana na utunzaji na usimamizi na uwekzaji wa fukwe pamoja na mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi inayohusiana na usimamaizi wa fukwe nchini.
Bw.Singo ameeleza kwamba dhima ya mwaka huu katika kongamano hilo inalenga kufungua majadiliano katika kuelekea kupata suluhisho la namna Madhubuti ya kusimamia na kuwekeza katika fukwe za bahari, maziwa na mito nchini ili ziweze kutoa tija katika ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Amesema dhima imezingatia dhamira ya dhati ya serikali inayolenga kuimarisha uchumi wan chi pasipo kuharibu mazingira.