Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Uwekezaji ya Uingereza (BII) Nick O’Donohoe na ujumbe wake, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Dodoma.
Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameipongeza Taasisi hiyo kwa kuendelea kuwekeza nchini tangu mwaka 1949 katika sekta muhimu na za kipaumbele kwa uchumi wa Taifa ikiwemo Nishati, Kilimo na Chakula, Misitu, Huduma za Fedha, Huduma za Mawasiliano pamoja na kushirikiana na Benki za Tanzania ikiwemo Benki ya NMB.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mkazo katika kuendelea kufungua uchumi kwa kufanya mageuzi muhimu yanayochochea na kuvutia biashara na uwekezaji. Ameongeza kwamba Serikali imeendelea kufanya mageuzi ya kisera kwa kuhakikisha sera na sheria zinazotabirika. Aidha, Serikali inaendelea kufanya mageuzi ya kitaasisi ili kuhakikisha mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa salama.
Amesema Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya changamoto mbalimbali zinazoikumba dunia kwa sasa.
Vilevile, amewakaribisha kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda misitu na mazingira kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Uwekezaji ya Uingereza (BII) Bw. Nick O’Donohoe amesema Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Nishati hususani nishati ya jua na upepo. Pia kuunga mkono uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji umeme, Kilimo pamoja na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya mbogamboga na maua.
Bwana O’Donohoe amesema nchi ya Tanzania imekua moja ya nchi zenye uchumi imara na unaokuwa kwa kwa kasi na hivyo kuvutia wawekezaji. Ameishukuru Serikali kwa mazingira wezeshi kwa Taaasisi hiyo katika kutekeleza miradi mbalimbali.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Taasisi ya BII Afrika Bw. Chris Chijuitomi na Mkuu wa Mipango Bw. John Trees. Ujumbe wa Tanzania ni pamoja na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Nyongo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mhe. Mbelwa Kairuki pamoja na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomaisa ya Kiuchumi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga.