Home Kitaifa MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AHIMIZA KUBORESHA AFYA NA MIUNDOMBINU YA...

MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AHIMIZA KUBORESHA AFYA NA MIUNDOMBINU YA SOKO LA TANDIKA

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema maendeleo ya Taifa yanategemea, kwa kiasi kikubwa, ustawi bora wa Jamii pamoja na afya njema kwa Wananchi wote

Mheshimiwa Othman  ameyasema hayo mapema  Leo Novemba 01 2024, alipotembelea Soko la Tandika, Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa afya za Wananchi zikiimarika, huchangia kwa kiasi kikubwa, hamasa na uwezo wao wa kufanya-kazi, hali ambayo hupelekea ongezeko la  uzalishaji-mali, pamoja na nguvu-kazi ya Taifa.

Akigusia ubovu wa Miundombinu ya Soko hilo, hali ambayo amesema katu haikubaliki, Mheshimiwa Othman amehoji akisema, “jee, mkiona watu wanakimbilia hospitali kwaajili ya kupata matibabu, hiyo inatokana na nini? kwamba wamepatwa na maradhi ambayo huenda miongoni mwao ni kwasababu ya haya haya mazingira machafu tunayoishi”.

Hivyo, pamoja na kuahidi kuzichukua na kuzifanyia-kazi changamoto za takriban Wafanyabiashara Mia Saba (700) wa Maeneo hayo, Mheshimiwa Othman amesema ni Wajibu wa Serikali kuhakikisha kunakuwepo Hatua za Haraka, ili kunusuru mazingira ya sasa, ambayo hayaendani kabisa na hadhi ya Soko hilo.

Kwa upande wao, Makamu Mwenyekiti wa Soko hilo, na Katibu wake, Bw. Abdirahman Jongo, na  Bw. Ahmad Liule, wameeleza changamoto mbali mbali, ambazo wamesema siyo tu zinadhoofisha juhudi za kuleta maendeleo, bali pia ni tishio kwa usalama wa maisha yao ya kila siku.

Wamebainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na Uchakavu Mkubwa wa Miundombinu; Uchafu Uliokithiri hapo; Ukosefu wa Vyoo; na kwamba pia Mamlaka zimeshindwa kuhurumia hata kulirekebisha Paa la Soko hilo ambalo ni bovu kupindukia, licha ya Watendaji kurandaranda hapo muda wote wakikusanya Kodi.

Nao, Wafanyabiashara wa hapo, Bw. Haruna Ramadhan, na Geudence Mkude, wamesema wamechoshwa na ahadi za  kila siku, kutoka kwa Wasimamizi wa Halmashauri, bali wanachoshuhudia ni kuendelea kudhoofika kwa miundombinu ya Soko hilo, kadiri maisha yanavyokwenda, wakihisi kama kwamba limetelekezwa.

Mara baada ya Ziara hiyo Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni  Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, amekutana na kufanya mazungumzo  na Viongozi na Wagombea wa Chama hicho, wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Mwishoni mwa Mwezi huu wa Novemba, Tanzania Bara yote.

Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa ‘Temeke Lodge’, uliopo pia hapo hapo Tandika, Jijini Dar es Salaam.

Viongozi mbali mbali wamejumuika katika Kikao hicho, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Upande wa Tanzania Bara, Ndugu Isihaka Rashid Mchinjita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!