Home Kitaifa MAHIZA AZIONYA NGOs ZINAZOKIUKA MAADILI

MAHIZA AZIONYA NGOs ZINAZOKIUKA MAADILI

Na Mwaandishi wetu Kilimanjaro

Muktasari:Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, Mwantumu Mahiza, amesema kumekuwapo na ongezeko la mashirika yanayokiuka maadili kwa kisingizio cha kusaidia jamii.

Moshi.Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, Mwantumu Mahiza, ameyataka mashirika hayo (NGOs) kufanya kazi kwa mujibu wa malengo yao ya usajili na kuacha kuhamasisha ajenda zinazokiuka maadili ya Kitanzania.

Mahiza anetoa rai hiyo leo Februari 18,2025 wakati wa mkutano wa viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali uliofanyika mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambapo amesema kumekuwapo na ongezeko la mashirika yanayokiuka maadili kwa kisingizio cha kusaidia jamii.

“Kila shirika lililosajiliwa lifanye kazi kwa mujibu wa lengo lake. Uzoefu umeonyesha kuwa baadhi ya mashirika yamesajiliwa kwa shughuli fulani, lakini utekelezaji wake unaenda kinyume na maadili yetu kwa kuingiza ajenda zisizo sahihi,” amesema Mahiza.

Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa na changamoto kubwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita hali ambayo imetokana na baadhi ya mashirika kushiriki shughuli zisizozingatia mila na desturi za Taifa.

“Tanzania hii ni yetu, hatuwezi kukubali mashirika yatumike kuharibu maadili ya vijana wetu. Kama kuna shirika linaloendelea na ajenda hizo, ni vyema likaacha mara moja kwa sababu ni kinyume cha sheria na maadili yetu,” amesisitiza Mahiza.

Mahiza ametaja kampeni zinazoendelea kama “My body, my right” na “My body, my choice” kuwa zinakwenda kinyume na utamaduni wa Kitanzania kwa kudhoofisha mamlaka ya wazazi katika malezi ya watoto wao.

Aidha Mahiza amewataka viongozi wa mashirika hayo kutanguliza uzalendo na kuhakikisha shughuli zao haziathiri maadili ya taifa.

“Tanzania ni nchi ya amani, tunapoelekea uchaguzi mkuu mashirika yasitumike kuvuruga utulivu wetu. Wote tunapaswa kushirikiana katika kujenga nchi yenye maadili na kizazi chenye heshima kwa tamaduni zetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala amesema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kukumbushana wajibu wa mashirika na kuhakikisha yanafuata mwongozo wa maadili katika utendaji wake.

“Mashirika yasiyo ya kiserikali yana mwongozo wa maadili unaosimamia utendaji wake. Ni muhimu kila shirika kuhakikisha linazingatia mwongozo huu ili kulinda heshima ya kazi tunayofanya kwa jamii,” amesema Makala.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu, amesema Mkoa huo una mashirika 467 yaliyosajiliwa, lakini yenye uhai kisheria ni mashirika 177 pekee.

“Changamoto kubwa ni kwamba mashirika mengi hayawasilishi taarifa za utekelezaji wa shughuli zao kila robo mwaka kama sheria inavyotaka. Serikali haina dhamira ya kuyakandamiza, bali kuhakikisha yanafanya kazi kwa mujibu wa sheria,” amesema Nzowa.

Aprili 2023, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Same ilisitisha mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na taasisi moja (jina limehifadhiwa) baada ya kubaini yalikuwa na maudhui yaliyokiuka maadili. Mafunzo hayo, yaliyodaiwa kuwa ya afya ya jamii, yalibainika kutumia vitabu na picha zisizofaa, kinyume na mwongozo wa serikali.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kupitia ibara za 154, 155 na 157, inaeleza bayana kuhusu makosa ya kinyume cha maumbile, jaribio la kujamiiana kinyume cha maumbile, pamoja na matendo ya aibu baina ya wanaume. Masharti haya yanaungwa mkono na Sheria Na. 47 ya mwaka 1954, kifungu cha 3, pamoja na marekebisho ya mwaka 1998 chini ya kifungu cha 16, 17, 18 na 19.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!