Na Shomari Binda – Musoma
MWENYEKITI wa kundi la WhatsApp la jamii ya Wana Musoma, Benedict Magiri, amesema kuwa kusudi lake pamoja na viongozi wenzake ni kulifanya kundi hilo kuwa na malengo makubwa zaidi ya kuchangia msiba na kuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kijamii.
Magiri alisema kuwa moja ya malengo makuu ya kundi hilo ni kupata viti 500, tents 4, na vyombo vya muziki vitakavyosaidia katika shughuli mbalimbali za umoja huo, na kwamba kila mwanajamii atakayekutana na tukio la msiba au shughuli nyingine muhimu atapata vifaa hivyo.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akimkabidhi rambirambi ya shilingi milioni 3.6 kwa mwana jamii Selemani Keraba, aliyefiwa na mama yake mzazi.
Akiwa anazungumza, Magiri alisema kuwa kwa kipindi cha miaka 8, kundi hilo limekuwa likichangishana katika matukio mbalimbali ya msiba, kuanzia kwa michango midogo hadi kufikia kiwango cha juu, ikiwa ni zaidi ya milioni 3. Ameongeza kuwa malengo yao ni kuendelea kuimarisha mchango wa kijamii kwa kuwa na vifaa muhimu vitakavyosaidia katika matukio ya kijamii.
“Katika harakati hizi, tutaanza kukusanya vifaa hivyo kupitia harambee itakayofanyika Februari 21, kwenye hafla ya umoja wetu itakayofanyika katika ukumbi wa Mwembeni Complex,” alisema Magiri.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa hafla hiyo, ambayo hufanyika kila mwaka, itahudhuriwa na mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na Mjumbe wa Baraza Kuu la CCM, Fadhil Maganya, pamoja na wageni wengine mbalimbali.
“Leo tumekuja kumfariji ndugu yetu Keraba baada ya kufiwa na mama yake mzazi, lakini makusudi ya umoja huu ni kuwa na malengo makubwa zaidi na kuhakikisha tunawaunga mkono wanajamii wetu katika nyakati ngumu,” alisisitiza.
Selemani Keraba, akizungumza kwa niaba ya familia, alishukuru kwa mchango wa rambirambi na kusema kuwa amefarijiwa na msaada wa jumuiya. Alisema mchango huo unadhihirisha umoja wa jamii na msaada wa kweli kwa wale wanaopita katika misukosuko ya maisha.
Akipokea ujumbe wa shukrani kutoka kwa wana jamii, Mkurugenzi wa Le Grand Hotel, Rama Msomi, alisisitiza kuwa umoja wa Wana Musoma umekuwa mfano wa kuigwa katika kuungana na kusaidiana, na akawashukuru viongozi wa kundi hilo kwa juhudi zao za kuunganisha watu na kuwa kitu kimoja