–ATAKA TOFAUTI ZA VIONGOZI ZISIWEPO
–AOMBA WAMUACHE AMSAIDIE RAIS SAMIA KAZI
Na Shomari Binda-Musoma
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Fadhil Maganya amewataka wana CCM kushikamana na kuendelea kukiimarisha chama.
Kauli hiyo ameitoa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Musoma mjini wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi kwenye jimbo la Musoma mjini.
Amesema hakuna kitu kizuri katika shughuli za kisiasa kama kuwa na ushirikiano mzuri kwa viongozi na wanachama ili kuendelea kushika dola.
Maganya amesema kutokuwa na ushirikiano huibua migogoro jambo ambalo halitarajii na kuwataka viongozi na wanachama kuwa wamoja.
Amesema zipo taarifa za kutofautiana kidogo kwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Musoma mjini Benedict Magiri na mbunge Vedastus Mathayo wa jimbo la Musoma mjini na kuwataka kuwa kitu kimoja..
Maganya amesema lipo jukumu la kuhakikisha kuona CCM inapata ushindi kuanzia ngazi za serikali za mitaa mwakani na ni muhimu kuwa na ushirikiano.
“Bila kuwa na ushirikiano ndugu wanachama hatuwezi kukojenga chama na kubwa ni kuondoa makundi na kuwa kitu komoja.
“Rais wetu Dkt.Samia jambo ambalo halipendi ni makundi ndani ya chama kama yapo hapa Musoma mjini yajifute yenyewe na tukijenge chama.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Wazazi amepongeza tukio la mapatano ya Mbunge na Mwenyekiti na kila mmoja kuonyesha hakuna tofauti na kuwa tayari kufanya kazi za chama.
Wakati huo huo Maganya smewataka wana CCM kuacha kutengenezeana ajali ambazo hazina maana ili kuangushana kisiasa.
Amesema analo jukumu la kumsaidia kazi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wenye nia mbaya wamuache aendelee kumsaidia kazi kupitia nafasi ya Mwenyekiti wa Wazazi Taifa.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha miaka mitatu 2020/2021 hadi 2023 na kudai serikali anayoiongoza Rais Samia imetoa fedha nyingi kwaajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya Elimu,Afya,Miundombinu pamoja Maji.
Amesema fedha hizo zimeweza kusaidia ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari katika jimbo la Musoma mjini pamoja na kuongeza madarasa.
Wajumbe wa mkutano huo mkuu wa CCM wilaya ya Musoma mjini wamempongeza mbunge huyo kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kutekeleza ilani ya uchaguzi.