
Na Deborah Lemmubi-Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahsusi ma nne kwa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ikiwemo kusimamia Donda sugu la migogoro ya Ardhi na kuwataka Viongozi hao kutojiingiza katika Migogoro hiyo kwani Migogoro ya Ardhi inaua,inaleta uhasama na pamoja na kuwepo kwa madhara mengine.
Rais Dkt Samia ameyasema hayo leo hii Jijini Dodoma Machi 11,2025 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT).

Na kuwataka kuimarisha mifumo ya Kitaasisi na kushughulikia kero na malalamiko ya Wananchi kwa wakati kwani Wananchi ndio waajiri wao hivyo wakafanye kazi itakayowaridhisha na kuendelea kujenga imani juu ya wananchi hao.
“Maelekezo mahsusi kwa ALAT muendelee kusimamia Watumishi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaaili watoe huduma bora ambazo zinakidhi mahitaji ya wananchi,tuwapokee,kuwasikikiza na kuwahudumia wananchi kwa Weledi,Hekima na Busara”.

“Pili imarisheni mifumo ya Kitaasisi nanuwezo wa Viongozi na Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi kwa wakati kwani wananchi ndio waajiri,twendeni tukafanye kazi waridhike ili waendelee kutuweka“.
“Pia ongezeni juhudi katika kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha makusanyo katika vyanzo vilivyopo“.

“Migogoro ya Ardhi ndio donda sugu kwenye maeneo yetu na mingine tunaisababisha sisi wenyewe Viongozi,sasa nendeni mkaisimamie,rekebisheni na toeni suluhisho katika Migogoro ya ardhi,Migogoro hii inaua watu,Migogoro inaleta uhasama,Migogoro ina madhara mengi sana,sasa kwanza Viongozi tusijiingize katika Migogoro ya Ardhi lakini pia tukasimame kwenye haki ili mwenye haki apate na aso haki aambiwe Huna haki”.
Aidha Dkt Samia amewataka Watendaji wa Mamlaka ya serikali za mitaa wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wale wenye nia ya kugombea katika Chaguzi zijazo za 2025 kutoa Taarifa mapema juu ya nia zao ili watu wa chini yao wapandishwe katika nafasi zao na sio kuchukua fomu na kuacha Serikali za Mitaa zikiwa hazina Viongozi wala Wasimamizi wenye uzoefu, Na kutoa tahadhi kwamba wasipofanya hivyo itawapelekea wao kukosa nafasi zote.
Mkutano huu wa ALAT ni wa 39 na umeongozwa na kauli mbiu isemayo:”Shiriki katika Uchaguzi Mkuu 2025 kwa Maendeleo Endelevu “.