Na Shomari Binda-Musoma
MADIWANI wa Halmashauri ya Musoma vijijini wamesikitishwa na kina dada wanaoendelea kujihusisha na biashara ya ngono.
Wakizungumza kwa hisia kali kwenye kikao cha robo ya tatu ya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo wamesema hali ni mbaya na hatua zinapaswa kuchukuliwa.
Wakichangia kwenye taarifa ya kamati ya kudhibiti UKIMWI wamesema bila kuwa makini nguvu kazi ya taifa itapotea kwa kupata maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.
Moja ya eneo ambalo limetajwa kuwepo kwa wanaojihusisha na biashara hiyo ya ngono ni Busekera na kuhitajika kupelekwa kwa elimu.
Diwani wa viti maalum kutoka Kata ya Mugango Kadogo Kapi amesema linapoongelewa suala la udhibiti wa UKIMWI haitakiwi aibu katika kuzungumzia.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Charles Magoma amesema kila diwani kwenye Kata yake anapaswa kuitisha vikao na kuzungumzia suala la maambukizi ya UKIMWI.
Amesema biashara ya ngono itakomeshwa kama elimu itatolewa na kila mmoja kutambua athari zake.
Akitoa salamu za serikali kaimu mkuu wa Wilaya ya Musoma ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Butiama Mwalimu Moses Kaegere amesema suala la ukusanyaji wa mapato ni muhimu katika kuendesha halmashauri.
Amesema uwepo wa uchumi utasaidia hata katika mapambano dhidi ya Ukimwi na kuitaka kamati kuendelea kufanya kazi ya kudhibiti.
Amedai kuwa biashara ya ngono haikubaliki na serikali inapiga marufuku na madiwani wa Musoma vijijini wanapaswa kusimama imara katika mapambano dhidi ya UKIMWI.