TAASISI ya Lions Club imetoa msaada wa matanki nane ya kuhifadhia maji kwa ajili ya shule za Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze.
Akisoma taarifa ya Taasisi hiyo Muntazir Bharwani kwa niaba ya Mwenyekiti wa Lions Club Host Kaniz Naghavi alisema hafla hiyo imeambatana na kumkaribisha Gavana wa Tanzania District 411C Happiness Nkya katika shughuli za chama .
Amesema wametoa matanki hayo pamoja na vyakula kwa watoto yatima Kidogozero baada ya kupokea maombi kutoka kwa Diwani wa Vigwaza Mussa Gama.
Amewaomba wakazi wa Vigwaza kuhifadhi na kuyatumia vizuri matanki hayo Ili yaweze kuwasaidia wanafunzi na kuwaondoa katika tatizo la kukosa maji wakiwa shule.
Taasisi hiyo imetoa hamasa kwa taasisi nyingine kutoa huduma na misaada kwa wanafunzi wa Shule za hapa nchini kutokana na uhitaji wa vitu vingi utaratibu ambao utasaidia kuboresha masuala ya elimu, afya na michezo.
Gavana wa Taasisi hiyo Hapiness Nkya alisema kwasasa wapo wanachama 620 na club 23 huku 14 zikiwa Dar es Salam wamekuwa wakitoa misaada kwenye maeneo mbalimbali ambayo wanashiriki moja kwa moja na mingine kuomba kwenye makampuni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze Ramadhani Poss, Afisa Elimu awali na Msingi wa Halmashauri hiyo aliishukuru taasisi hiyo kwa misaada ambayo inaitoa kupunguza vikwazo kwa wakazi wa Vigwaza.
Diwani wa Vigwaza Mussa Gama ameishukuru Taasisi hiyo huku akieleza kwamba umekuwa ikisaidia mambo mbalimbali ya maendeleo katika Kata hiyo kwa kutoa vifaa kwenye Zahanati, daftari kwa wanafunzi na sasa matanki na vyakula kwa yatima.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ruvu Darajani Samwel Mjema alisema matanki hayo yanakwenda kuwasaidia kutunza maji pindi yanapokatika huku akiahidi kuyatunza Ili yadumu kwa muda mrefu na kuwa msaada kwa wanafunzi.
Matanki hayo nane ni kati ya kumi ambayo yanatolewa katika shule za Sekondari na Msingi Kata ya Vigwaza kwa ajili ya kuhifadhia maji safi na salama kwa matumizi ya wanafunzi shuleni.
Mwisho.