Home Afya SERIKALI INAENDELEZA JUHUDI ZA KUPUNGUZA VIFO VYA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA-WAZIRI UMMY

SERIKALI INAENDELEZA JUHUDI ZA KUPUNGUZA VIFO VYA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA-WAZIRI UMMY

Na. WAF – Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendeleza juhudi za kupunguza viwango vya vifo vya wajawazito na watoto wachanga kwa kuzingatia mipango bora ya afya ya uzazi.

Hayo ameyasema leo Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akipokea wodi ya wazazi iliyokarabatiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na vitanda vya kujifungulia kutoka Benki ya NMB vyenye thamani ya shilingi Milioni 300.

Nitoe shukrani zangu za dhati kwa Benki ya NMB kwa ukarabati huu wa wodi ya wazazi na watoto wachanga ambao umegharimu kiasi cha shilingi Milioni 250 na vifaa tiba (vitanda vya kujifungulia) vilivyogharimu kiasi cha shilingi Milioni 50.” amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema Wodi hiyo ya wazazi iliyokarabatiwa na vitanda vipya vya kujifungulia vitasaidia sana katika kuboresha utoaji wa huduma kwa akina mama na watoto wao.

Katika kutambua umuhimu wa Sekta binafsi Waziri Ummy ameziomba Sekta hizo kuendelea kufanya uwekezaji katika sekta ya afya ili kuendelea kuboresha Afya za wananchi na hatimaye kuimarisha uchumi na kujenga Tanzania yenye maendeleo endelevu.

Aidha, Waziri Ummy ametoa rai kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutumia vifaa hivyo vipya kwa uangalifu na kwa umakini pia amewakumbusha kuandaa mpango endelevu wa matengenezo kabla havijaharibika (PPM).

Sambamba hilo Waziri Ummy amesema huduma bora zinazoendelea kutolewa zimepelekea kupunguza Vifo vya Watoto chini ya miaka mitano kutoka 67 kati ya vizazi hai 1000 mwaka 2015/16 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000 pamoja na mahudhurio ya kliniki ya wajawazito mara nne na Zaidi kutoka 53% hadi 65%.

Ikumbukwe kuwa, huduma bora na salama kwa Mama na Mtoto ni kipaumbele cha juu kabisa cha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na mimi nitakisimamia vizuri ili tuweze kupunguza vifo vya mama na mtoto.” amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika afya ya mama na mtoto kwa kujenga vituo vya afya, kununua vifaa tiba na dawa Pamoja na kuajiri watumishi wa afya na kupeleka watumishi hao katika vituo hivyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!