Home Kitaifa KUELEKEA CHAGUZI ZA SERIKALI ZA MITAA WANACCM WAANZA KUJIPANGA

KUELEKEA CHAGUZI ZA SERIKALI ZA MITAA WANACCM WAANZA KUJIPANGA

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinyishehe Mlao amewataka wanaCCM kujenga Umoja na msikamano kuelekea chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji Hadi uchaguzi Mkuu mwakani ili CCM ipate ushindi wa kishindo na kuendelea kubaki madarakani.

Amesema hayo wakati wa kilele Cha sherehe za maadhimisho ya Miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM mkoa wa Pwani huko Katika Kijiji Cha Fukayosi Wilaya ya Bagamoyo ambapo wanaCCM mkoa mzima walikusanyika na shughuli mbalimbali za utekelezaji wa Ilani zilifanyika.

Amesema wanaCCM waendelee kujenga Umoja na msikamano na kuacha tabia ya ubinafsi ili kujenga Chama Cha Mapinduzi na ilikuweza kuendelea kudumu madarakani lazima Viongozi waondoe ubinafsi.Amesema unapofika wakati wa uchaguzi Kila mpiga kura ahakikishe anawachagua Viongozi wa Serikali wenye nia njema ya kuongoza na ikitokea wakawachagua Viongozi kwa ajili ya maslahi yao binafsi basi watakuwa wamepoteza haki za wengine.

Amefafanua kuwa ili kushinda chaguzi zijazo kunahitajika UMOJA huku akisisitiza kuwa kama Kuna mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea na anaonekana kuwa na dosari aambiwe sasa wasisubiri mpaka achukue fomu ndio waseme mabaya yake huko ni kuchafuana.

“Tusikubali kusababisha migogoro isiyo na tija tunapoelekea kwenye chaguzi zijazo na wala tusikubali watu watugawe kwa ajili ya maslahi yao”* amesema Mlao

Maadhimisho hayo yameambatana na ukaguzi wa Kituo Cha afya cha Fukayosi kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1, Uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi ya CCM kata ya Fukayosi, ugawaji wa vifaa vya Shule kwa wanafunzi wanaoishi katika Mazingira magumu, ugawaji wa vyeti vya PONGEZI kwa Kata zilizofanya vizuri katika uingizaji wanachama wapya na usajili kwa mfumo wa kielektroniki sambamba na zoezi la upandaji wa miti.

Awali akimkaribisha Mwenyekiti huyo Katibu wa CCM mkoa wa Pwani Bernard Ghati amesema sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM mkoani Pwani zilianza tangu tarehe 28 mwezi wa kwanza ambapo uzinduzi ulifanyika katika Kata ya Mlanzi wilayani Kibiti.

Ghati amesema shughuli mbalimbali za utekelezaji wa Ilani zilifanyika ikiwa ni pamoja na kushiriki ujenzi wa Ofisi za Chama na jumuhia zake, ukaguzi wa miradi ya maendeleo, usafi katika maeneo ya taasisi za umma kuanzia ngazi ya mkoa, Wilaya, Kata, vijiji kwenye mashina na matawi ya CCM kwa ushirikiano wa wanaCCM na serikali.

Katika sherehe hizo Mwenyekiti wa CCM huyo wa mkoa wa Pwani alikabidhi sare za shule, madaftari, peni kwa Wanafunzi walio katika mazingira magumu na watoto yatima wa Shule za msingi na Sekondari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!