Home Biashara KONGAMANO LA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA UMOJA WA ULAYA KUWAKUTANISHA ZAIDI...

KONGAMANO LA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA UMOJA WA ULAYA KUWAKUTANISHA ZAIDI YA WASHIRIKI 600.

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya pamoja na Sekta Binafsi ya Tanzania imeandaa Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 hadi 24 Februari, 2023 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema kongamano hilo linatarajiwa kujumuisha zaidi ya washiriki 600 kutoka nchi za Umoja wa Ulaya na Tanzania linalenga kuwaunganisha washiriki hao ili kuwawezesha kubadilishana uzoefu, kushirikiana na watoa maamuzi na kukutana na wawekezaji wanaofaa pamoja na kujenga uelewa kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo kwa sekta ya umma na binafsi ambapo, hati za makubaliano mbalimbali ya Uwekezaji baina ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya zitatiwa saini.

Akizungumzia uzinduzi wa kongamano hilo Dkt. Kijaji amesema linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, akimwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na litafungwa rasmi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi ambaye atashuhudia utiaji saini wa mikataba ya fedha na hati za makubaliano.

Aidha Mhe. Waziri amesema kongamano hilo litahudhuriwa na Mawaziri nane (8) kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mabalozi sita (6) wa Tanzania katika nchi za Umoja wa Ulaya ambao watashiriki katika vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Biashara.

“Ninatarajia kuona kongamano hili la Biashara la kwanza kuwa fursa ya kuvutia wawekezaji, teknolojia na utalaamu katika nchi yetu na kuvutia biashara na uwekezaji kutoka duniani kote katika sekta za nishati, madini na kilimo endelevu.” hivyo tunatarajia hati za makubaliano zitakazotiwa saini zitaendeleza na kukuza biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, zitaongeza ajira kwa vijana na zitachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, amesema Dkt. Kijaji.

Aidha,. Mhe. Dkt. Kijaji amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania watumie fursa hiyo vizuri kuendeleza na kukuza biashara yao kwa kujifunza mbinu mpya za kibiashara, kupata wabia na masoko ya bidhaa zetu nje ya nchi.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari Mhe. Waziri aliongozana na Naibu Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Emilio Rossetti, Balozi wa Ufaransa Nchini Mhe. Nabil Hajlaoui pamoja na Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF) Bi. Kinanasy Seif.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!